SIKU chache baada ya Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo kueleza kiu ya serikali ya kuona nchi inaondokana na mgawo wa umeme, kudhibiti kukatikakatika kwa umeme, kuzalisha umeme wa uhakika na unaotabirika kwa maendeleo ya viwanda, lakini pia kuwa na umeme nafuu, Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) limekuja na majibu ya hoja hizo, huku likisisitiza kuwa umeme utapanda kwa wateja wa kati na si wa chini.


Majibu hayo yalitolewa juzi usiku kwenye kipindi cha Kipima Joto kinachorushwa hewani na Kituo cha televisheni cha ITV na Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco Felchesmi Mramba, huku akishuhudiwa na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (EWURA), Felix Ngamlagosi, aliyetoa pia ufafanuzi wa masuala kadhaa.

Hatua hiyo imekuja ikiwa ni wiki moja kupita tangu Ewura ilipopokea maombi kutoka Tanesco ya kutaka kuongeza bei ya umeme kwa wastani wa asilimia 18.19 kwa mwaka 2017.

Katika maelezo yake ya juzi usiku, Mramba alisema kutokana na shirika hilo kuwajali wateja wa kipato cha chini, wateja hao hawataathirika na mapendekezo ya bei mpya, na badala yake watabakia na bei iliyopo sasa.

Mkurugenzi huyo pia alisisitiza kuwa shirika hilo halina mpango wa kurudisha tozo ya kuunganishiwa umeme ya Sh 5,000 na gharama ya huduma kwa kila mwezi ya Sh 5,520 ambazo ziliondolewa mwezi Aprili mwaka huu. Mapendekezo ya kupandisha bei ya umeme

Akifafanua mapendekezo hayo, Mramba alisema bei za umeme zinazotumika, zinatakiwa kutumika hadi Desemba 31, mwaka huu na baada ya hapo Januari mwakani sheria inataka bei mpya zitolewe. Alisema pamoja na mapendekezo hayo, walichoomba ni kuongezeka kwa bei kidogo ambayo haiwezi kuwaumiza wananchi, bali itaboresha zaidi huduma na kufanya wazipate kwa uhakika kama alivyoagiza Waziri Muhongo.

“Tanesco ilitakiwa kufanya tathmini ya gharama za uzalishaji, usafirishaji na usambazaji umeme na kupeleka mapendekezo hayo Ewura, ili kupitiwa na wadau, sasa suala la kupanda au kushuka kwa bei itategemea na mapitio ya tathmini ya gharama za kuzalisha, kusafirisha na kusambaza tulizowasilisha Ewura,” alisema Mramba.

Akizungumzia kuhusu kuondolewa kwa tozo ya gharama za kila mwezi pamoja na tozo ya kuunganishiwa umeme kwa wateja wapya, Mramba alisema katika mapendekezo hayo tozo hizo hazipo na wala hawana mpango wa kuzirudisha na kwamba wateja wa chini wao wataendelea kununua umeme kwa bei iliyopo sasa.

DOWNLOAD APP YETU YA SWAHIBA NEWS ILI UWEZE KUPATA HABARI ZOTE MOJA KWA MOJA KUPITIA SIMU YAKO YA MKONONI BILA KUINGIA KWENYE WEBSITE,KUDOWNLOAD BONYEZA HAPA  

ANDIKA MAONI YAKO HAPO CHINI
ads
Bonyeza HAPA kudownload applicationi ya SWAHILI NEWS kwenye simu yako ili kupata habari zetu Haraka
Share To:

SWAHIBA MEDIA STAFF

Habari , karibu katika mtandao wetu ili kuhabarika na stori zote za siku katika lugha yetu adhwim ya kiswahili, habarika wakati wote weka dunia kiganjani mwako na swahili news

Post A Comment: