SIKU moja baada ya mkazi wa Dar es Salaam, Said Mrisho aliyetobolewa macho kukabidhiwa msaada wa fedha na ahadi ya vitega uchumi, wafanyabiashara wameeleza kuwa akitumia vizuri msaada huo, atajipatia Sh milioni moja kila wiki.
Mrisho aliyetobolewa macho kwa visu Septemba 6 na mtu anayedaiwa
kuwa Henjewele Salum ‘Scorpion’ (34), juzi alipewa msaada wa Sh milioni 12,
pikipiki tano, bajaji mbili na ahadi ya kununuliwa nyumba.
Bajaji
Wafanyabiashara wa bajaji walisema hesabu ya chombo hicho kibiashara
ni Sh 15,000 kwa siku, hivyo Mrisho kwa kila moja atakuwa anaingiza Sh 105,000
kwa wiki sawa na Sh 210,000 kwa bajaji mbili kwa wiki.
Dereva na mmiliki wa bajaji anayefanya shughuli zake kwenye kituo
cha Sinza, Emmanuel Dito alisema kwa hali aliyonayo Mrisho, ni vema asitoe
vyombo vyake kwa mkataba, badala yake awape madereva watakaomletea hesabu ya
siku, ili vyombo hivyo vimlinde kwa muda mrefu.
“Mimi namshauri kijana mwenzangu atafutiwe wasimamizi wa uhakika
watakaokuwa waaminifu, ili adumu na vyombo vyake kwa muda mrefu lakini pia
ahakikishiwe anakatiwa bima kubwa kwa vyombo vyake vyote kwa ajili ya kuvilinda
zaidi,” alisema.
Loti Sadiki, dereva wa bajaji, alisema kazi hiyo kwa upande
mwingine ni ngumu kwa kuwa kuna baadhi ya maeneo kama mjini hawaruhusiwi
kuingia na kutokana na usalama, mara nyingine wanalazimika kulaza vyombo mapema
na kusababisha hesabu kuwa ngumu kutimia.
Bodaboda
Madereva na wamiliki wa pikipiki za biashara maarufu kama bodaboda,
walisema kwa siku pikipiki moja inaingiza Sh 7,000 hivyo kwa siku sita itakuwa
ni Sh 42,000 na kwa idadi ya pikipiki tano alizokabidhiwa ataingiza Sh 210,000
kwa wiki.
Said Kitindi, dereva wa bodaboda Mwenge, alishauri Mrisho asikubali
kutoa pikipiki kwa madereva kwa mikataba, kwa maelezo kuwa mfumo huo mara
nyingi unatumiwa na watu wenye biashara zao.
Kwa mujibu wa Kitindi, wanaotumia mfumo wa mkataba fedha za vyombo
hivyo huingia katika mzunguko wa kila siku wa biashara zingine, lakini kwa hali
aliyonayo Mrisho, ni vema atunze vyombo hivyo na achukue hesabu kila siku kwa
muda mrefu ili vimsaidie.
Dereva mwingine wa bodaboda, Zuberi Omary hakuwa mbali kimawazo na
wenzake, akipendekeza Mrisho apokee hesabu yake kwa siku au wiki, ili ajikimu
kimaisha kwa muda mrefu, tofauti na mkataba ambao ukifika mwisho, atapata ugumu
kiasi wa kupata pikipiki nyingine.
Mafundi
Mafundi wa bodaboda na bajaji, walisema vyombo hivyo vinavyotumika
kila siku huhitaji matengenezo ya hapa na pale, hivyo ili vifanye kazi kwa muda
mrefu, ni lazima vipate matengenezo hayo.
Mohamed Yassir, fundi wa bajaji na pikikipi, alisema matengenezo ya
bodaboda ni mara moja kwa wiki, ambapo gharama zake hazizidi Sh 10,000 na kwa
upande wa bajaji, ni mara mbili kwa mwezi na gharama yake ni Sh 15,000.
Saluni
Kuhusu biashara aliyozoea ya kunyoa nywele, Mrisho alishauriwa kama
akiwekeza kwenye biashara hiyo, ana uwezekano wa kuanzisha saluni za kisasa
mbili na kuvuna kipato kizuri kwa wiki.
Mmoja wa vinyozi wa Gongo la Mboto, Hamad Chande alisema saluni
moja huwa na viti vinne na kila kiti na kinyozi wake atakayetakiwa kumlipa Sh
90,000 kwa wiki Sinza na Sh 50,000 kwa wiki Buguruni.
Kwa mujibu wa Chande, kwa saluni za Sh 90,000 kwa kiti, Mrisho anaweza
kujipatia Sh 360,000 kwa wiki na kwa Sh 50,000, atajipatia Sh 200,000.
DOWNLOAD
APP YETU YA SWAHIBA NEWS ILI UWEZE KUPATA HABARI ZOTE MOJA KWA MOJA
KUPITIA SIMU YAKO YA MKONONI BILA KUINGIA KWENYE WEBSITE,KUDOWNLOAD
BONYEZA HAPA
ANDIKA MAONI YAKO HAPO CHINI
Post A Comment: