BUNGE limeendelea kuibana serikali itekeleze agizo la kuondoa kodi kwenye tende, ili kuwawezesha waumini wa dini ya Kiislamu kupata bidhaa hiyo kwa urahisi katika kipindi cha mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.
Naibu Spika wa Bunge, Dk. Tulia Ackson, aliigiza serikali kufanyia kazi agizo hilo alipotolea ufafanuzi mwongozo ulioombwa kwake Hamidu Bobali bungeni jijini hapa jana asubuhi.
Mbunge huyo wa Mchinga (CUF), alisimama na kuomba Bunge liahirishe shughuli zake za jana na kujadili hoja hiyo kwa muda wa dakika 30 kwa kuwa licha ya wabunge kadhaa akiwamo Mbunge wa Ubungo (Chadema), Saed Kubenea na Mbunge wa Nzega (CCM), Hussein Bashe kuiomba serikali iondoe kodi kwenye tende katika vikao vilivyopita, bado haijatekeleza.
Alisema tende katika nchi za Kenya, Zanzibar na Msumbiji zimefutiwa kodi katika kipindi cha kuelekea mfungo huo, lakini Tanzania bado haijachukua uamuzi huo.
“Sasa, Mwezi wa Ramadhani unaanza wiki ijayo na makontena yapo kwenye meli bandarini ambayo yametolewa kwa msaada wa mali za wakfu, watu wanajichangisha mali za wakfu zinaletwa na wao wanatafuta swawabu. Sasa naliomba Bunge walau nusu saa, kwa sababu jambo hili linaiaibisha Tanzania,” alisema.
Akimjibu mbunge huyo, Dk. Tulia alisema kuwa jambo hilo limeshazungumzwa na utaratibu wake upo kisheria, hivyo serikali ina wajibu wa kuliangalia.
“Nadhani serikali ifanyie kazi jambo hili ione namna bora ya kushughulikia, kama ambavyo Bobali ametaja mifano ya huko kwingine sijasoma sheria zao, lakini sheria tunatunga wabunge, ila watekelezaji serikali, upande wa watekelezaji mwangalie namna ya kushughulikia jambo hili ili Mwezi wa Ramadhani unapokuja, wenzetu wenye imani ya Kiislamu waweze kupata hizo huduma ambazo zipo kiutaratibu," alisema.
Post A Comment: