Ikiwa unatumia matokeo ya vipimo vya Virusi vya Ukimwi kupitia mahudhurio ya kliniki za ujauzito wa mke wako, inabidi ujitafakari upya.


“Kati ya mwaka 1998 hadi 1999, nilikuwa nikiugua maradhi ya zinaa mara kwa mara na wakati huo nilikuwa naishi na mwanamke mwingine tofauti na mke wangu ambaye alikuwa Morogoro kikazi na mimi nilikuwa naishi Njombe,” anaanza kwa kusimulia hivyo, Justine Mwinuka.

Katika mahojiano maalumu na gazeti la  Mwananchi mapema wiki hii, Mwinuka aliyefunga ndoa na Aneth Mdong’ala (49), anasema hakuwahi kufikiri kama wakati huo alikuwa ameambukizwa virusi vya Ukimwi.

Lakini ilipofika mwaka 2001, mwanamke huyo alifariki dunia na yeye aliendelea kushiriki tendo la ndoa na mke wake na miaka 10 baadaye, alijigundua kwamba ameathirika.

Anasema awali baada ya mwanamke huyo kufariki dunia, minong’ono ya chini chini ilizungumzwa kwamba alikuwa ameathirika na ukimwi. Lakini anasema hata baada ya kusikia minong’ono ile hakufikiri kwenda kupima, kwani alihofia kupata majibu hasi baada ya kupima.

Lakini tangu aliporudi kwake, mkewe alikuwa na kawaida ya kwenda kupima virusi vya ukimwi mara kwa mara na alipopata majibu ya mkewe kuwa hana maambukizi, Mwinuka alikuwa akijifariji kwamba na yeye hana maambukizi.

“Kumbe nilikuwa najidanganya. Kwa mara ya kwanza nilipima virusi mwaka 2008, nikagundulika nina maambukizi,” anasema na kuongeza, “Ilinipa mawazo na fikra zisizo na majibu. Ndani ya miezi sita niliishi kwa shida sana, lakini kwa bahati nzuri mke wangu alikuwa mwepesi wa kunitia moyo, hofu yangu kubwa ilikuwa ni namna gani nitaweza kuishi na maambukizi haya,” anasimulia Mwinuka.

Hata hivyo, anasema baada ya kupatiwa elimu ya ushauri nasaha baada ya kujiunga na kikundi cha Faraja, hali yake ilianza kubadilika kwani alijikubali.

“Nikajikuta nimekuwa jasiri nisiyeogopa, lakini awali nilidhani hata mke wangu nilitakiwa nimuache, sikutaka kumuambukiza. Nilimpa wazo tutengane, lakini alinitia moyo na kuniambia tutaendelea kuishi naye na kweli tumeendelea kuishi hivi hadi leo tumepata mafanikio mengi katika maisha yetu,” anasema.

Akisimulia mkasa mzima, Aneth anasema kabla ya mumewe hajaenda kupima, alimuhisi ni mgonjwa baada ya afya yake kuanza kudhoofika kila kukicha.

Anasema alimshauri mumewe aende akapime afya mwaka 2008, wakati huo na yeye alikuwa akiendelea kupima kila baada ya kipindi fulani, lakini kila mmoja alienda kwa wakati wake.

Anasema siku moja mumewe alimuaga anakwenda kupima, na yeye wiki iliyofuata akaenda hospitali kupima pia.

“Alivyorudi hakunieleza alichoambiwa hospitali, ila alienda kwa mchungaji wetu akamwelezea, nadhani kuna kitu kilifanyika kwa kuwa alivyokuja akanieleza moja kwa moja majibu ya vipimo vyake, nilijisikia amani ya kuishi naye, kwa hiyo tukaendelea kuishi, mchungaji alitushauri tuwe tunapaka mafuta mengi kwenye sehemu zetu za siri tunapofanya tendo la ndoa, lakini mwenzangu alipoenda kituo cha afya ili kuomba msaada zaidi, wakamweleza siyo sahihi bali tunatakiwa tutumie kondomu,” anasema mama huyo.

Maisha ya familia

Akizungumzia maisha ya familia, Aneth anasema watoto wao watatu wanafahamu kuhusu hali zao kiafya na baada ya kulitambua hilo, hawakupata mshtuko kwa sababu wamekuwa wakiishi kwa amani, hivyo wameendelea kuwa na amani.

Anasema kwa upande wa ndugu jamaa na marafiki, pia wanalitambua hilo baada ya mumewe kuchaguliwa kuwa kiongozi wa watu wanaoishi na virusi vya Ukimwi kitaifa.

Je alizipokeaje taarifa za mumewe kuathirika

Anasema taarifa za mume wake kuathirika hazikumshtua sana, “tulitoka Njombe mwaka 1995 kuhamia Morogoro, huko tumeishi kwa miaka sita wakati anaondoka kwenda Njombe tena, aliniacha nikiwa na mtoto wa mwezi mmoja na nusu, kwa hiyo tangu 1998 hadi 2000, alikuwa akiishi na yule mke mwenzangu na mimi nilirudi Njombe 2001 na mwaka huohuo, Yule mama alifaraiki dunia.”

Anasema aliwahi kupima afya yake mwaka 2003 kwa agizo la mchungaji, lakini hakupatikana na maambukizi, akapima tena mwaka 2008 ikaonekana hana, hivyo ameendelea kupima hadi mwezi wa tisa mwaka huu, bado damu yake inaonyesha hana maambukizi.

Mwanamke huyo anayejivunia kuwa mama bora wa familia yake anasema, yeye ni mwalimu wa Shule ya Msingi Igelehedza na amekuwa akifanya kazi hiyo tangu 1987.

“Mume wangu tangu awali ni mkulima na mfugaji, lakini kwa sasa amechaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Baraza la Watu wanaoishi na Virusi vya Ukimwi Taifa,” anasema Aneth.

Anasema licha ya mumewe kuathirika, bado wanazungumza namna ya kujilinda ili kuepusha maambukizi mapya.

“Tumeambizana, huenda alipata maambukizi kutokana na mwenendo wake wa zamani lakini sasa inabidi abadilike, na sasa anamjua Mungu, inabidi tuishi maisha yanayompendeza. Maneno hayo yamemsaidia maana angekuwa nje ya imani huenda angeendeleza tabia ya awali.”

Je anatumia dawa za kufubaza virusi vya Ukimwi?

Anasema mumewe baada ya kugundulika ana maambukizi, alinzishiwa dawa za kufubaza makali yaani (ARV).

Lakini pia kama mke, anajitahidi anampikia vyakula vizuri vinavyompatia lishe ya kutosha ili kumuepusha na maradhi nyemelezi.
ads
Bonyeza HAPA kudownload applicationi ya SWAHILI NEWS kwenye simu yako ili kupata habari zetu Haraka
Share To:

SWAHIBA MEDIA STAFF

Habari , karibu katika mtandao wetu ili kuhabarika na stori zote za siku katika lugha yetu adhwim ya kiswahili, habarika wakati wote weka dunia kiganjani mwako na swahili news

Post A Comment: