
HAIDER Gulamali, mwanaCCM aliyekuwa akiwania kumrithi aliyekuwa Mbunge wa Singida Kaskazini, Lazaro Nyalandu, alifikishwa kortini jana baada ya kukamatwa juzi mjini hapa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) akituhumiwa kutoa rushwa ya Sh. milioni mbili.
Akizungumza na gazeti la Nipashe kwa simu akiwa Dodoma jana jioni, Ofisa Uhusiano wa Takukuru Makao Makuu, Mussa Misalaba, alisema Gulamali alifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Singida jana mchana mbele ya Hakimu Flora Ndale na kusomewa mashtaka na Mwendesha Mashtaka wa Takukuru, Edson Mapalala.
Mshtakiwa ambaye kwa mujibu wa Misalaba ni mfanyabiashara wa viwanda vya magodoro mjini Dodoma, alikana mahakamani shtaka la kutoa rushwa juzi saa 8:30 mchana.
Misalaba alisema: "Mshtakiwa alikamatwa juzi kwa kutoa rushwa ya Sh. milioni mbili kwa Kiseo Nzowa, ili amsaidie kushinda uchaguzi Singida Kaskazini na alishapita kwenye kura za maoni."
Kwa mujibu wa Misalaba, mshtakiwa anatetewa na Wakili wa Kujitegemea, Godfrey Wasonga.
HATIMA YA DHAMANAOfisa huyo wa Takukuru aliongeza kuwa upande wa mashtaka ulipinga mshtakiwa kupewa dhamana kwa maelezo kuwa atavuruga mchakato wa uchaguzi licha ya kwamba chama chake tayari kimeshatengua ushindi wake alioupata katika kura za maoni.
Misalaba alisema kesi hiyo iliahirishwa hadi leo Mahakama itakapotoa uamuzi kama mshtakiwa anastahili dhamana au la.
ALIVYOKAMATWA
Awali jana asubuhi Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Singida, Joshua Msuya, aliwaeleza waandishi wa habari mjini hapa jinsi walivyomnasa mfanyabiashara huyo.Alidai walimkamata mjini hapa kwa tuhuma za kutoa rushwa ya Sh. milioni mbili baada ya kumwekea mtego.
Gulamali, mkazi wa Dodoma, alishinda kwenye kura za maoni zilizopigwa Jumapili akiwania kiti hicho kilichobaki wazi baada ya Nyalandu kujiuzulu na kuomba kuhamia upinzani Oktoba.
Ilielezwa na 'kigogo' huyo wa Takukuru kuwa mwanaCCM huyo kabla ya kufikishwa kortini jana mchana, alikuwa anashikiliwa kwa tuhuma ya kumpatia rushwa ofisa usalama wa taifa mmoja ili amsaidie kuthibitishwa na vikao vya juu.
Msuya aliwaambia waandishi wa habari ofisini kwake kuwa Gulamali alikamatwa juzi saa nane alasiri kwenye hoteli moja mjini hapa akiwa na ofisa huyo.
“Tunamshikilia Haider Hussein Gulamali, alishawishi kumpa rushwa ofisa usalama wa taifa," alisema Msuya na kwamba "aliendelea kuwasiliana naye, lakini kutokana na mtego tuliouandaa, tulimkamata baada ya kukabidhi fedha hizo Sh. milioni mbili.”
Alisema kukamatwa kwa mtia nia huyo kulitokana na kupata taarifa iliyotaka ofisa huyo akamtolee habari nzuri kwenye ngazi za juu ili athibitishwe na vikao husika kugombea Jimbo la Singida Kaskazini kwa tiketi ya CCM.
Mkuu huyo wa Takukuru alisema uchunguzi zaidi unaendelea na utakapokamilika, Gulamali atafikishwa mahakamani haraka iwezekanavyo kujibu tuhuma zinazomkabili.Aidha, Msuya alisema uchunguzi zaidi unaendelea kufuatilia tuhuma za vitendo vya rushwa dhidi ya mtuhumiwa anavyodaiwa kufanya kabla na baada ya upigaji kura za maoni Jumapili.Nyalandu, waziri wa zamani wa Maliasili na Utalii, alitangaza kuachia ubunge wa Sindiga Kaskazini na kuihama CCM Oktoba 30 kisha kujiunga na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kutokana na kile alichodai kutoridhishwa na mwenendo wa sasa wa chama hicho tawala.
Lakini siku mbili baadaye, taarifa ya Spika wa Bunge, Job Ndugai, ilieleza kuwa hakupokea barua ya Nyalandu kujiuzulu nafasi yake.
Aidha, Ndugai alisema alichopokea ni barua kutoka kwa Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, ya Oktoba 30 ikimwarifu kuwa Nyalandu amepoteza sifa ya kuwa mwanachama wa chama hicho na ubunge kwa mujibu wa ibara ya 13 ya katiba yao.
Kutokana na taarifa ya Kinana, Ndugai aliiarifu Tume ya Uchaguzi (NEC) kuwa jimbo la Singida Kaskazini lipo wazi.
Post A Comment: