UPANDE wa Jamhuri umepokea jalada kutoka kwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) dhidi ya kesi ya utakatishaji wa Dola za Marekani 300,000 inayowakabili Rais wa klabu ya soka ya Simba, Evans Aveva na Makamu wake, Godfrey Nyange maarufu kama ‘Kaburu’ likiwa na maelekezo ya kuendelea upelelezi.
Kesi hiyo ilitajwa jana mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi wa Mahakama ya Kisutu, Victoria Nongwa. Wakili wa Serikali Mwandamizi, Leonard Swai, alieleza kesi hiyo ilipangwa kwa ajili ya kutajwa, lakini upelelezi wake haujakamilika.
Alidai DPP amerejesha jalada na ametoa maelekezo upelelezi zaidi uendelee.
“Mheshimiwa hakimu upande wa Jamhuri tunaomba ufunguo kutoka kwa mshtakiwa wa kwanza Aveva, ili tuweze kupata nyaraka mbalimbali kama sehemu ya kukamilisha upelelezi wa kesi hii... Aveva alikuwa na ofisi mbili ya Simba na binafsi na katika ofisi binafsi kuna nyaraka za klabu hiyo,” alidai Swai.
Alidai upande wa Jamhuri ulimwandikia barua gerezani ili awapatie funguo kwa kupata nyaraka zinazohitajika, lakini hawajajibiwa.
Aliomba upande wa utetezi uharakishe wapate nyaraka kukamilisha upelelezi. Wakili wa utetezi, Evodius Mtawala, akijibu maombi hayo alidai Aveva ameipata barua hiyo na juhudi zinaendelea kukusanywa na zitawasilishwa karibuni.
Hakimu Nongwa alisema kesi hiyo itatajwa tena Desemba 28 na pande zote zikamilishe taratibu hizo ili kesi iendelee.
Katika kesi ya msingi, Aveva na Kaburu wanakabiliwa na mashtaka matano ya kughushi, kuwasilisha nyaraka ya uongo na kutakatisha dola hizo.
Wakati huo huo, kesi inayowakabili waliokuwa vigogo wa Shirikisho la Soka Tanzania(TFF) akiwamo, Jamal Malinzi imeahirishwa hadi Desemba 28.
Hakimu Mkazi Mkuu,Thomas Simba, aliagiza upande wa mashtaka kukamilisha upelelezi haraka.Washtakiwa wengine kwenye kesi hiyo ni aliyekuwa Katibu Mkuu, Mwesigwa Celestine na Mhasibu, Nsiande Mwanga.
Wanakabiliwa na mashtaka 28, yakiwamo ya utakatishaji fedha wa Dola za Marekani 375,418.
Post A Comment: