KESI inayomkabili Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema (Chadema) ya madai uchochezi dhidi ya Rais John Magufuli, imezidi kupigwa kalenda.
Hatua hiyo ilijitokeza tena jana baada ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Arumeru, Desderi Kamugisha, anayesikiliza kesi hiyo kutokuwapo mahakamani hapo.
Akiahirisha kesi hiyo jana mbele ya Wakili wa Serikali Alice Mtenga, Hakimu Mkazi Patricia Kisinda alisema kesi hiyo haiwezi kuendelea sababu hakimu anayesikiliza kesi hiyo hayupo.
“Kesi hii ilikuja leo kwa ajili ya usikikilizwaji lakini haiwezi kusikilizwa kwa sababu hakimu wenu anayesikiliza hayupo, hivyo naipanga Januari 18, mwakani,” alisema.
Oktoba 9, mwaka huu, Wakili Sheck Mfinanga, alijitoa kuendelea kumtetea mteja wake kwa kile alichodai kuomba mwenendo wa kesi zaidi ya mara tatu mahakamani hapo na kushindwa kupewa ili kukata rufani Mahakama Kuu, lakini Hakimu Kamugisha amegoma kutoa.
Awali, wakili Mfinanga alimwomba Hakimu Kamugisha kujitoa kusikiliza kesi ya hiyo licha ya mbunge huyo kumtaka afanye hivyo kwa kile alichodai kuwa aliwahi kufanya uamuzi wa hila uliosababisha kukaa mahabusu kwa zaidi ya miezi minne.
Hata hivyo, hakimu huyo aliamua kuendelea na shauri hilo, hata pale mawakili wa Lema walipowasilisha kwa mdomo kusudio la kukata rufani Mahakama Kuu kwa lengo la kupinga uamuzi huo wa kuendelea kusikiliza kesi hiyo.
Hata hivyo, Wakili wa Serikali, Khalili Nuda, aliiomba mahakama itupilie mbali hoja hizo kwa kuwa anaamini hakimu alitoa uamuzi kwa kuzingatia sheria, huku akidai kuwa mawakili wa Lema wana nia ya kuchelewesha usikilizwaji wa kesi.
akitolea uamuzi mdogo hoja hizo, kamugisha alisema hazina mashiko hivyo kuzitupa, kwa kile alichoeleza kuwa jaji au hakimu hawezi kujitoa kwa sababu za kudhaniwa, kufikirika au zinazotokana na uoga.
Post A Comment: