LICHA ya timu yake kuwa kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Kocha Mkuu wa Simba, Mcameroon Joseph Omog, amesema hajafurahishwa na pointi alizonazo katika mechi tano alizocheza za ligi hiyo inayotoa mwakilishi wa nchi katika mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.


Simba ambayo inadhaminiwa na Kampuni ya Kubashiri Matokeo ya SportPesa, huku ikiwa mabingwa wa Kombe la FA, ina pointi 11 sawa na Azam FC na Mtibwa Sugar, na imepoteza pointi nne ambazo zilitokana na sare mbili walizopata dhidi ya Azam FC na Mbao FC.

Akizungumza na gazeti la nipashe, Omog, alisema anahitaji kuongoza ligi huku akiwa na tofauti ya pointi zaidi ya tano ili kujihakikishia kumaliza mzunguko wa kwanza akiwa kwenye nafasi hiyo muhimu inayowaniwa na timu 16 zinazoshiriki ligi hiyo.

Omog alisema mawazo na akili yake ni kuhakikisha wanashinda mechi zao zinazofuata.

"Tulipoteza pointi mbili tulipocheza na Azam na tulipokwenda Mwanza vile vile, haikuwa jambo jema, lakini ndiyo matokeo ya mpira yalivyo, tunahitaji kuhakikisha hatupotezi tena pointi licha ya kuwa mechi zote ni ngumu," alisema Omog.

Aliongeza kuwa jana asubuhi nyota wake wote walifanya mazoezi kwa ajili ya kujiandaa na mechi dhidi ya Mtibwa Sugar itakayofanyika Jumapili kwenye Uwanja wa Uhuru jijini.

"Mechi zote ni muhimu na tutaingia uwanjani kuendelea kusaka ushindi, tunaziheshimu klabu zote kwa sababu wote tunashiriki ligi moja, tunapoingia uwanjani tunakuwa kwenye hadhi moja, hapo ndipo heshima ya kila upande inatakiwa kuonekana katika kusaka matokeo mazuri," Omog aliongeza.

Alisema kwa kiwango kikubwa kila idara kwenye kikosi hicho imefanya kazi nzuri, lakini kama timu inahitaji kuona wanaongeza bidii katika mechi zote zinazofuata.

Baada ya mchezo huo wa Jumapili dhidi ya Mtibwa Sugar inayofundishwa na Kocha Zuberi Katwila, kikosi hicho kitaendelea kufanya mazoezi ya kuikaribisha timu mpya iliyopanda daraja ya Njombe Mji na Oktoba 28 watakuwa wageni wa Yanga, mechi zote zikifanyika kwenye Uwanja wa Uhuru.
ads
Bonyeza HAPA kudownload applicationi ya SWAHILI NEWS kwenye simu yako ili kupata habari zetu Haraka
Share To:

SWAHIBA MEDIA STAFF

Habari , karibu katika mtandao wetu ili kuhabarika na stori zote za siku katika lugha yetu adhwim ya kiswahili, habarika wakati wote weka dunia kiganjani mwako na swahili news

Post A Comment: