Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe amesema kauli ya Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki, Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Polycarp Kardinali Pengo kuhusu mchakato wa Katiba imewasikitisha.


Wakati Mbowe akitoa kauli hiyo, mwenyekiti wa kamati ya kitaifa ya maadili, amani na haki za binadamu kwa jamii ya madhehebu ya dini zote Tanzania, Askofu William Mwamalanga amemshauri Rais John Magufuli kuufufua mchakato huo uliokwama.

Mbowe, ambaye pia ni Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni akizungumza jana baada ya kuombwa kutoa maoni yake kuhusu msimamo wa Kardinali Pengo kwamba Katiba siyo kipaumbele chake, bali huduma za jamii, Mbowe alisema Askofu huyo ni kiongozi wa dini anayepaswa kulinda heshima aliyonayo ndani na nje ya kanisa.

Katika taarifa yake ya kufafanua kauli iliyotolewa na Askofu wa Jimbo la Rulenge mkoani Kagera, Severine Niwemugizi baada ya kukaririwa akisema kwamba Katiba Mpya ndiyo kipaumbele cha wananchi, Kardinali Pengo alisema hayo yalikuwa maoni yake binafsi siyo msimamo wa Kanisa Katoliki nchini.

“Mtu akiniambia priority (kipaumbele) ya Tanzania ni Katiba Mpya inabidi anithibitishie huo ukipaumbele maana siwezi kuona mtoto anakufa kwa njaa au kwa kukosa dawa eti kwa sababu ya Katiba Mpya. Kwangu mimi Katiba ni kitu ambacho kije baadaye, si cha haraka.

“Wanasiasa wasiache watoto wetu wafe kwa njaa kisa malumbano ya Katiba. Wasiache watoto wakose shule kwa sababu hela zote zimeishia kwenye malumbano juu ya Katiba,” alisisitiza Kadinali Pengo.

Lakini jana akizungumzia msimamo huo, Mbowe alisema, “Askofu Pengo ni kiongozi wa kanisa, anaheshimika na wananchi ambao si wale anaowaongoza tu lakini kwa kauli yake kuhusu Katiba, imetushangaza na imenisikitisha,” alisema Mbowe na kuongeza:

“Suala la elimu, chakula na maisha yetu yanalindwa na Katiba, ndiyo msingi wa mifumo ya rasilimali za Taifa. Anaposema haoni umuhimu wa Katiba anatufikirisha, anataka kusema mchakato wa Katiba uliogharimu mabilioni ya fedha leo hauna maana?”

Mbowe alisema umefika wakati mchakato wa Katiba uliokwama ukaendelezwa na hasa kuanzia katika rasimu ya Katiba iliyoandaliwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba chini ya mwenyekiti, Jaji mstaafu Joseph Warioba.

“Katiba ni maridhiano, tunahitaji kupata maridhiano ya pande zote, nirudie tu kwamba alichokisema Askofu Pengo kinasikitisha.”
ads
Bonyeza HAPA kudownload applicationi ya SWAHILI NEWS kwenye simu yako ili kupata habari zetu Haraka
Share To:

SWAHIBA MEDIA STAFF

Habari , karibu katika mtandao wetu ili kuhabarika na stori zote za siku katika lugha yetu adhwim ya kiswahili, habarika wakati wote weka dunia kiganjani mwako na swahili news

Post A Comment: