ads

TUNASEMA ni mechi ya historia na kisasi, hayo ni maneno ya Kocha Mkuu wa timu ya Zanzibar (Zanzibar Heroes), Hemed Suleiman "Morocco" kuhusiana na mechi yao ya hatua ya nusu fainali ya Kombe la Chalenji dhidi ya Uganda (Cranes) itakayofanyika kuanzia saa 9:00 mchana kwenye Uwanja wa Moi.


Akizungumza  jana, Morocco, alisema kuwa mchezo wa leo dhidi ya mabingwa watetezi utakuwa mgumu na wenye ushindani kwa sababu kila timu inahitaji kutinga fainali na ina wachezaji wanaojua kupambana kusaka ushindi.

Morocco alisema kuwa licha ya kuwakosa wachezaji wake wawili wa kikosi cha kwanza ambao ni pamoja na beki, Haji Mwinyi mwenye kadi mbili za njano na mshambuliaji tegemeo, Kassim Suleiman, bado ana nyota wengine watakaoziba nafasi zao vizuri.

"Ni kweli tutakuwa na pengo kumkosa Haji Mwinyi, lakini tuna kikosi kipana ambacho kinauwezo wa kucheza kama wenzao, tunajua mchezo wa nusu fainali unahitaji matokeo, tutacheza kwa kushambulia na vile vile kuzuia kwa umakini," alisema Morocco.

Aliongeza kuwa watacheza mfumo kulingana na malengo na mipango watakayoingia nao wapinzani wao Uganda.

"Tumejiandaa vizuri kimwili na kiakili, tunajua itakuwa mechi ngumu kwa sababu tunacheza na wachezaji wazoefu hivyo tunatakiwa kupambana zaidi kwa sababu malengo yetu ni kuchukua kikombe cha ubingwa mwaka huu," alisema nahodha wa Zanzibar Heroes, Suleiman Kassim "Selembe".

Naye Kocha wa Cranes, Moses Basena, alisema kikosi chake kiko imara na kitaingia uwanjani huku kikifahamu wazi wachezaji wa Zanzibar Heroes ni wapambanaji.

" Tunajua kesho tutaingia uwanjani kucheza na timu nzuri, ilipata matokeo mazuri katika kundi lake na muhimu ina wachezaji wanaojua kupambana kwa ajili ya kutengeneza maisha yao na baadhi wanacheza Ligi ya Tanzania Bara," alisema Basena.

Aliwataja wachezaji wake wawili ambao atawakosa katika mechi ya leo kutokana na kutumikia kadi nyekundu kuwa ni pamoja na Mulemee Isaack na Awadhy Timothy.

Fainali za mashindano haya zitafanyika keshokutwa katika Uwanja wa Kenyatta ulioko kwenye mji wa Machakos, Kenya ambao utatanguliwa na mchezo wa kusaka mshindi wa tatu.

Kenya yatangulia fainali

Katika nusu fainali ya kwanza iliyochezwa jana jioni, wenyeji timu ya taifa ya Kenya ilitangulia fainali baada ya kushinda bao 1-0 dhidi ya Burundi.

Kenya sasa inasubiri mshindi wa leo kati ya Uganda na Zanzibar kufahamu mpinzani wake kwenye mchezo wa fainali.
ads
Bonyeza HAPA kudownload applicationi ya SWAHILI NEWS kwenye simu yako ili kupata habari zetu Haraka
Share To:

SWAHIBA MEDIA STAFF

Habari , karibu katika mtandao wetu ili kuhabarika na stori zote za siku katika lugha yetu adhwim ya kiswahili, habarika wakati wote weka dunia kiganjani mwako na swahili news

Post A Comment: