Polisi Wilaya ya Arusha imepiga marufuku mikutano ya hadhara ya Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema kwa maelezo kuwa kutakuwa na ujio wa viongozi wa kitaifa jijini hapa.


Pia, kuzuiwa mikutano ya mbunge huyo wa Chadema kumeelezwa kuchangiwa na kuungua moto kwa nyumba za polisi kwa kuwa jeshi hilo limeelekeza nguvu kubwa huko.

Barua iliyoandikwa jana na Mkuu wa Polisi Wilaya ya Arusha, Mrakibu Mwandamizi wa Polisi, E.Tille kwenda wa Lema inaeleza kuwa mikutano yake iliyokuwa ifanyike jana na leo imesitishwa.

Kwa kuwa siku hizo zina mwingiliano na ratiba za shughuli za kiserikali za viongozi wa juu wa Serikali inayoishia Oktoba 4.

Pia amesema janga la moto katika kambi ya Polisi lililotokea juzi usiku limeleta madhara makubwa hivyo, nguvu kubwa itaelekewa huko.

“Unashauriwa kupanga mikutano yako tarehe yoyote kuanzia Oktoba 5, 2017 pia rejea mazungumzo yangu na wewe ofisini kwangu ya tarehe 29/09/2017,” inasomeka barua hiyo.

Hata hivyo, Lema amepinga polisi kuzuia mikutano yake akisema ni ukiukwaji wa sheria na haki za mbunge.

Alisema Sheria ya Bunge, Kifungu cha Nne, Fasili ya kwanza, kinazungumzia uhuru wa mbunge kufanya mikutano jimboni kwake na Kifungu cha 4(1) na (2) vinaelezea uhuru huo wa mbunge kufanya mikutano na pia ni ukiukwaji wa sheria kuzuia mikutano yake kwenye jimbo lake.

Alisema anaamini, kuzuiwa kwa mikutano yake ni njama kwa kuwa awali alipanga kuzungumza na wananchi wa Kata ya Kimandolu ambako diwani wao amejiuzulu na kisha wananchi wa Mjini Kati.

“Kwanza waliniita wakaniambia hali ya kisiasa si nzuri nisiende kufanya mkutano Kimandolu kwa kuwa wananchi wanaweza kuwa na hasira baada ya diwani kujiuzulu, mimi nikawaambia wasiwe na hofu lazima likafanye mkutano,” alisema.

Alidai kwamba polisi wanaamini atazungumzia sakata la kupigwa risasi Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu na pia ziara ya Rais John Magufuli jijini Arusha hivi karibuni na kwamba anashauriana na wanasheria wake kuona kama akubali barua ya polisi au aendelee na mikutano yake.

Hii ni mara ya pili kwa Lema kuzuiwa kufanya mikutano. Agosti 25 alizuiwa ili kupisha mbio za Mwenge wa Uhuru na mitihani ya darasa la saba na alitii agizo hilo.
ads
Bonyeza HAPA kudownload applicationi ya SWAHILI NEWS kwenye simu yako ili kupata habari zetu Haraka
Share To:

SWAHIBA MEDIA STAFF

Habari , karibu katika mtandao wetu ili kuhabarika na stori zote za siku katika lugha yetu adhwim ya kiswahili, habarika wakati wote weka dunia kiganjani mwako na swahili news

Post A Comment: