
Subscribe ndio neno gumu zaidi kwa wabongo kuliko kutafuna jiwe kama ilivyo kwa Waingereza kutamka Mwanjelwa..husema Monjela
Pamoja na vionjo hivyo..kwenye Simba Day ya mwaka huu ntakuja na style tofauti ya kutambulisha wachezaji...njoo ushuhudie mwenyew..usingoje kuhadithiwa ni Jtano hii pale dimba la Taifa... #SimbaDay #KibingwaZaidi 🇵🇪🇵🇪
Serikali yatoa tamko kuadimika mafuta ya kula nchini
Waziri Kigwangalla atetea ununuzi wa ndege
Zitto Kabwe amshauri Job Ndugai
Bunge lataka tende zifutwe kodi mfungo wa Ramadhani
Mo Dewji afunguka jinsi anavyopiga pesa kupitia kilimo
WAKATI msimu wa sikukuu za kuelekea mwishoni
mwa mwaka ukiwadia, mambo zaidi ya nane yametajwa kuwa ni ya kuchungwa
na kila mmoja ili furaha isibadilike na kuwa kilio.
Jeshi la Polisi kupitia msemaji wake, Kamishna Msaidizi wa Polisi na
Msemaji wa Jeshi hilo, Advera John Bulimba, lilitoa tahadhari za
kiusalama kuhusiana na sikukuu hizo mbele ya waandishi wa habari jana
huku pia wazoefu wa masuala ya biashara na wakuu wa dini wakitoa usia
wao kuhusiana na mambo muhimu ya kuzingatia ili sikukuu isiharibiwe kwa
habari mbaya za misiba na majanga.
Katika taarifa yao kwa umma, polisi walichimba mkwara mzito kwa
kuahidi kuchukua hatua za kisheria kwa wote watakaofurahia sikukuu hizo
kwa namna inayokiuka sheria na kuhatarisha usalama, huku Askofu Mkuu wa
Jimbo la Mahenge, Agapiti Ndorobo, akionya kuwa kila mmoja anapaswa
kuhakikisha kuwa hatendi mambo ya ovyo na kumchukiza Mungu.
Mhadhiri wa Uchumi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Joel Silas,
aliwashauri Watanzania kutumia vyema rasilimali zao katika kipindi hiki
ili sikukuu zikimalizika wasibaki bila kitu mikononi mwao.
Keshokutwa, Watanzania wataungana na watu wengine duniani kote
kusherehekea Krismasi kabla ya kufuatiwa na siku ya kupeana zawadi
(Boxing Day) katika siku inayofuata na mwaka mpya ifikapo mwisho wa
mwezi huu.
TAHADHARI YA POLISI
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Kamishna Bulimba alisema baadhi ya wahalifu hutumia vipindi vya sikukuu kufanya vitendo vya kihalifu, lakini akaonya kuwa yeyote atakayejaribu kufanya hivyo atachukuliwa hatua kali kwa sababu wamejipanga kuhakikisha kuwa amani na utulivu vinaendelea kudumishwa wakati wote.
“Tumejipanga vya kutosha, siwezi kuweka mbinu hadharani hapa kwa
sababu za kiusalama, lakini itoshe tu kuwaambia kwamba Jeshi la Polisi
liko vizuri na asithubutu mtu yeyote kufanya uhalifu mahali popote maana
tuna mkono mrefu… tutamkamata,” alisema Bulimba.
Aliwataka wananchi kutoa ushirikiano kwa kufikisha taarifa haraka
wanapobaini kuwa kuna mtu, kundi au watu wanaowatilia shaka, huku kila
mmoja akiwa mlinzi wa jirani yake katika biashara, makazi na mahali
pengine.
“Ukiona kuna mtu anaingia kwa jirani yako halafu humfahamu au
unamtilia shaka, mpigie simu au piga simu polisi kupitia namba 111 na
112,” alisema.
Aliongeza kuwa jeshi hilo limejipanga pia kwa kuimarisha ulinzi
katika maeneo ya kuabudia, sehemu za fukwe za bahari, sehemu za starehe
na maeneo mengine ambayo yatakuwa na mikusanyiko mikubwa ya watu.
Bulimba aliwataka waendeshaji wa kumbi za starehe kuzingatia uhalali
wa matumizi ya kumbi zao na kuepuka kuzidisha idadi ya watu tofauti na
uwezo wa kumbi zao na kwamba kwa yeyote atakayebainika kufanya hivyo
atachukuliwa hatua kali.
Kuhusu ulinzi katika barabara, Bulimba alisema jeshi hilo pia
limejipanga kudhibiti matukio ya kizembe ikiwamo madereva walevi na
kwamba wameandaa vituo vya polisi vya kuhamishika ambavyo vitawekwa
katika maeneo tofauti ili kuwarahisishia wananchi kuripoti moja kwa moja
matukio yanayotishia usalama wa raia na mali.
Aidha, Bulimba alikumbushia vilevile kuwa ni marufuku kusherehekea
sikukuu hizi kwa kupiga fataki, kuchoma matairi barabarani na kuandaa
‘disco toto’ kwa sababu matendo yote hayo ni uhalifu na wahusika
watachukuliwa hatua za kisheria.
Kwa ujumla, katika uchunguzi
mambo mengi ya kuzingatia, yapo takribani tisa ya msingi kuyakumbuka
katika kipindi hiki cha sikukuu za mwisho wa mwaka.
1. TUMIA FEDHA KWA MPANGO
Kati ya mambo muhimu ya kuzingatia kuelekea sikukuu ya Krismasi na pia zile za ‘Boxing Day” na Mwaka Mpya ni kutumia fedha kwa umakini. Tahadhari hii inatolewa kutokana na ukweli kuwa baada ya kumalizika kwa sikukuu hizo, hali huwa ngumu. Isitoshe, Januari ni mwezi unaombatana na changamoto nyingi.
“Kuna masuala ya kodi za pango, ada za watoto shuleni na majukumu
mengine mbalimbali. Yeyote yule asipokuwa makini, dunia yote ataiona
chungu na Januari ataiona ndefu. Ni muhimu kukumbuka kuwa kuna maisha
baada ya sikukuu hizi,” mmoja wa wafuatiliaji wa masuala ya kiuchumi
aliiambia Nipashe jana.
Akizungumzia hilo, Dk. Silas alisema ni lazima Watanzania wabadilishe
muundo wa maisha kwa kuelekeza matumizi ya fedha katika mambo ya msingi
kwa kuepuka kuishi kwa mazoea.
2. ZINGATIA SHERIA BARABARANI
Hili ni eneo jingine la kuchunga sana, hasa kwa madereva na watu wengine watakaosafiri kutoka eneo moja hadi jingine kwa nia ya kufurahia sikukuu.
Kwa mujibu wa Polisi, ajali nyingi zinazotokea katika kipindi cha
kuelekea mwisho wa mwaka husababishwa na watu wanaopuuza sheria za
usalama barabarani, hasa kwa kuendesha vyombo vya moto kwa kasi kubwa na
pia kujazana kwenye vyombo hivyo kupita kiasi.
Wapo pia wanaotembea kwa miguu barabarani bila ya uangalifu. Ili
kutimiza ndoto ya kuuona mwaka mpya, kila mmoja anapaswa kuzingatia
sheria awapo barabarani.
3. ULEVI KUPITILIZA NI KUITA KIFO
Ulevi wa pombe kupitiliza kwa baadhi ya madereva ni chanzo kimojawapo kikubwa cha ajali za mwisho wa mwaka. Baadhi ya ajali hizi zilisababishwa na ulevi na hivyo, ni muhimu kujua kuwa unywaji holela ni sawa na kujiweka karibu na kifo au ulemavu wa kudumu.
4. ACHA MICHEPUKO, IPE RAHA FAMILIA
Viongozi wa dini, akiwamo Askofu Ndorobo, wanasisitiza juu ya upendo kwa familia, na hasa katika kipindi kama hiki cha kuelekea sikukuu. Kwa sababu hiyo, inashauriwa kuwa ni vizuri kwa kila mmoja kuachana na wapenzi wa nje ya ndoa na badala yake kufurahi na familia. Madhara ya kutenda kinyume chake ni pamoja na kuyumbisha ndoa baada ya sikukuu hizi kumalizika.
Askofu Ndorobo alisema ni vyema Watanzania wakajenga utaratibu wa
kufurahi kwa pamoja kwenye matukio ya kifamilia kama kumbukumbu za siku
za kuzaliwa, maisha ya ndoa miaka mitano na zaidi na sherehe nyinginezo,
na kwamba kwa kufanya hivyo yatapunguza maovu mengi kwenye jamii.
5. USILE BATA PEKE YAKO, WAKUMBUKE YATIMA
Inashauriwa kwa kila mmoja kuwakumbuka yatima, masikini, walemavu na watu wengine wenye mahitaji maalumu na siyo kufaidi sikukuu na watu wachache wa familia peke yake. Lengo kubwa katika hili ni pamoja na kusambaza upendo, kuleta furaha kwa kila mmoja walau katika sikukuu hizi.
6. UMAKINI UNUNUZI WA ZAWADI ZISIWE ‘FEKI’
Mama au baba wa familia anapokwenda dukani kununulia bidhaa za zawadi kwa ajili ya sikukuu anapaswa kuwa makini wakati wote kutokana na mrundikano wa bidhaa bandia katika baadhi ya maeneo. Kwenda kufanya manunuzi holela kunaweza kuwasababishia kero wapendwa wako badala ya kuwaletea furaha iliyokusudiwa. Umakini huu uwe maradufu.
7. USIACHE WATOTO PEKE YAO KUOGELEA, DISCO
Kati ya makosa makubwa hufanyika katika siku za sikukuu ni pamoja na kuwaachia watoto waende kusherehekea siku hiyo kwenye maeneo mbalimbali bila ya uangalizi makini. Kwa mfano, ni hatari kuwaachia waogelee peke yao na pia siyo busara pia kuwaacha warundikane kwenye kumbi za disco, maarufu kama ‘disco toto’ wakiwa peke yao.
Kutozingatia maelekezo hayo yaliyosisitizwa jana na Jeshi la Polisi
ni sawa na kujiweka tayari kwa kulia na kusaga meno kutokana na taarifa
mbaya kuhusiana na usalama wa watoto.
“Kuna uzembe ambao huwa unafanywa na wazazi wa kuwaachia watoto kuzurula ovyo na wakati mwingine kuhatarisha maisha yao.
Sasa nataka ieleweke hivi, mzazi akibainika amezembea kumlinda mtoto
wake na akaletwa kituoni, lazima atakuwa na kitu cha kujibu na
tutamwajibisha,” alisema Bulimba na kuongeza:
“Kwa suala la disco toto, tulishalipiga marufuku. Halipo kabisa.”
8. EPUKA UCHOMAJI MATAIRI, ULIPUAJI FATAKI
Kusherehekea sikukuu kwa kuchoma matairi barabarani au kulipua mafataki kiholela ni miongoni mwa makosa makubwa yanayoweza kuharibu furaha na kuwa kilio kwa wahusika baada ya kukamatwa na kwenda kuwekwa mahabusu.
Bulimba alilikumbushia hilo jana na kuonya kuwa wakiukaji wa maelekezo hayo wajiandae kukamatwa na kuwekwa mbaroni.
9. KUMUOGOPA MUNGU
Jambo lingine muhimu ni kuendeleza amani kwa kufanya matendo yanayozingatia uwapo wa Mungu. Askofu Ndorobo alisema wapo watu waliozoea uhalifu kwa kutomhofia Mungu na hilo ni tatizo kubwa linalopaswa kufanyiwa kazi sasa na hata baada ya kipindi hiki.
“Kinachopungua kwa (baadhi ya) Watanzania ni hali ya kutomuogopa
Mungu kwa dhambi. Kila Mtanzania ni mlinzi wa mwenzake na pia ni mtunza
uhai wa mwenzake. Ndiyo maana kila mmoja akiheshimu uhai wa mtu… matukio
mabaya hayatatokea,” alisema Askofu Ndorobo.
DOWNLOAD
APP YETU YA SWAHIBA NEWS ILI UWEZE KUPATA HABARI ZOTE MOJA KWA MOJA
KUPITIA SIMU YAKO YA MKONONI BILA KUINGIA KWENYE WEBSITE,KUDOWNLOAD
BONYEZA HAPA
ANDIKA MAONI YAKO HAPO CHINI
Post A Comment: