
RAIS John Magufuli amesema Serikali ya Awamu ya Tano imedhamiria kufanikisha utafutaji na upatikanaji wa mafuta yaliyopo katika Bonde la Ufa la Eyasi Wembere na Ziwa Tanganyika, ili nchi ianze kunufaika na rasilimali hiyo.
Taarifa ya Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu ya jana ilisema Rais Magufuli aliyasema hayo muda mfupi baada kupokea taarifa ya maendeleo ya utafitii wa mafuta katika maeneo ya Bonde la Ufa la Eyasi Wembere na Ziwa Tanganyika, iliyowasilishwa na timu ya wataalamu wa Tanzania na Uganda.
Timu hiyo imeelezea uwepo wa viashiria vya uhakika vya kijiolojia vinavyothibitisha kuwepo kwa mafuta katika maeneo ya Senkenke, Mwanzugi na Kining'inila katika bonde la Manonga, wilaya ya Igunga mkoani Tabora.
Mkutano huo uliohudhuriwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi John Kijazi, Naibu Waziri wa Nishati na Madini Dk. Medard Kalemani na Balozi wa Uganda nchini, Richard Kabonero, taarifa ya Ikulu ilisema.
"Timu ya wataalamu hao imesema miamba, uoto na uwepo wa bonde la Eyasi Wembere katika mfumo mmoja wa bonde la Afrika Mashariki unaofanana na maeneo mengine yaliyothibitika kuwa na mafuta ni kiashiria muhimu cha kuwepo mafuta," taarifa hiyo ilisema.
"Kufuatia taarifa hiyo, Rais Magufuli amesema Serikali ya Awamu ya Tano ipo tayari kutekeleza shughuli zote zitakazowezesha kupatikana kwa mafuta katika bonde la Eyasi Wembere na Ziwa Tanganyika na amewaagiza wataalamu wa Tanzania kuendelea kufanya kazi kwa ukaribu na wataalamu wa Uganda ambao wana uzoefu wa kupata mafuta katika ziwa Albert nchini humo."
Taarifa ilisema Rais Magufuli aliwashukuru wataalamu wa Uganda wanaoshirikiana na wataalamu wa Tanzania katika kazi hiyo na amemuomba Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini wa Uganda, Robert Kasande kumfikishia shukrani zake kwa Rais Yoweri Museveni kwa ushirikiano anautoa katika kufanikisha upatikanaji wa mafuta nchini.
Post A Comment: