
RAIS John Magufuli ametoa mwito kwa Taasisi za Aga Khan kupunguza gharama za huduma zake kwa wananchi ili waweze kumudu, hasa ikizingatiwa kuwa zimekuwa zikipata msamaha wa kodi kutoka serikalini.
Rais Magufuli alisema hayo jana alipokutana Ikulu Dar es Salaam na Kiongozi wa Jumuiya ya Ismailia Duniani, Karim Aga Khan ambapo alimshukuru kwa taasisi zake kutoa huduma za kijamii hapa nchini.
Pia Rais Magufuli alieleza kuwa Serikali ya Awamu ya Tano ipo tayari kuendeleza na kuimarisha zaidi ushirikiano na Aga Khan na amemuomba kiongozi huyo kuendelea kupanua wigo wa huduma za taasisi zake, ikiwa ni pamoja na kuwekeza mjini Dodoma yaliko makao makuu ya Serikali.
Akizungumza na Rais, Aga Khan alisema Jumuiya ya Ismailia imedhamiria kuunga mkono juhudi za Serikali ya Awamu ya Tano kwa kupanua hospitali ya Aga Khan iliyopo Dar es Salaam na kujenga chuo kikuu kikubwa katika Afrika Mashariki mkoani Arusha.
Aga Khan alisema kuwa upanuzi wa hospitali ya Aga Khan, utahusisha kuongeza idadi ya vitanda vya wagonjwa kutoka 72 vya sasa hadi kufikia vitanda 172, utaimarisha matibabu ya moyo, kansa na utaongeza ufundishaji wa madaktari na wataalamu wengine wa afya.
Post A Comment: