ads

NI kishindo! Hivyo ndivyo inavyoweza kuelezwa kuhusiana na miezi 23 ya kuwa Ikulu kwa Rais John Magufuli na serikali anayoiongoza ya awamu ya tano.


Hadi sasa, katika kipindi hicho kinachoanzia Novemba 5, 2015, Serikali ya Rais Magufuli imeshafanya mambo kadhaa mapya kuonekana nchini katika miaka ya hivi karibuni, yakiwamo makubwa takribani 25.

Akihutubia katika Mkutano wa 33 wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa(ALAT) wa ALAT jijini Dar es Salaam jana, Rais Magufuli aligusia baadhi ya mambo hayo yaliyoacha kishindo cha aina yake.

Kwa mujibu wa Rais Magufuli jana, pamoja na uchambuzi wa gazeti la  Nipashe, mambo hayo ni pamoja na utekelezaji wa ahadi ya Magufuli ya kutoa elimu bure kwa kila Mtanzania kuanzia elimu ya msingi hadi kidato cha nne; vita dhidi ya vitendo vya rushwa na ufisadi; kudhibiti matumizi holela ya serikali ili fedha inayookolewa iwafikie wananchi wa kawaida kupitia miradi mbalimbali ya maendeleo na kufyeka mishahara mikubwa serikalini ukiwamo wake (Rais) ili kuendana na hali halisi pamoja na uwiano wa maslahi ya watumishi wa umma.

Aidha, mambo mengine yaliyofanyika katika kipindi hicho cha kuwa madarakani chini ya miaka miwili ya JPM ni pamoja na kuondoa kodi zilizoonekana kuwa kero kwa wananchi zikiwamo 80 kwa wakulima na saba kwa wavuvi; kuanza kwa ujenzi wa reli ya kisasa kiwango cha ‘standard gauge’; kuongezwa kwa mtandao wa barabara za lami nchini; kukomesha upotevu wa mapato ya serikali kwenye uchimbaji wa madini yakiwamo ya dhahabu, almasi na tanzanite; serikali kuhamia Dodoma; kuanza kwa ujenzi wa barabara za juu (flyovers) na ununuzi wa meli mpya.

Mambo mengine katika kipindi hicho ni kuongezeka kwa kasi ya ulipaji kodi; kufufua Shirika la Ndege (ATCL) kwa kununua ndege mpya; kudhibiti mfumuko wa bei; kukomesha upotevu wa fedha za umma kupitia mishahara kwa watumishi hewa; kuondoa watumishi wenye vyeti feki; kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi; kufyeka matumizi holela kama ya safari, warsha, semina na maadhimisho ya sherehe mbalimbali; kufanikisha uwapo wa madawati ya kutosha kwenye shule mbalimbvali za msingi na sekondari; kukomesha wizi katika ruzuku ya pembejeo za kilimo na utoaji fedha kwa kaya masikini hewa; kuongeza kasi ya vita dhidi ya ujangili na dawa za kulevya; kuanza kwa utekelezaji wa miradi mbalimbali ya umeme kama wa Stigler’s Gorge;
kuongezeka kwa kasi ya kuelekea uchumi wa viwanda; kuimarishwa kwa huduma za afya ikiwamo kuongeza vitanda wodini na pia ujio zaidi wa watalii na kuimarika kwa eneo la uwekezaji.

“Mwaka uliopita nchi yetu iliongoza kuvutia wawekezaji kwenye ukanda wa Afrika Mashariki… ripoti iliyotolewa na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AFDB) na UNDP (Shirika la Maendeleo la Umoja wa Taifa) inaitaja nchi yetu kuwa miongoni mwa zinazoongoza,” alisema Rais Magufuli jana wakati akielezea mafanikio katika uwekezaji.

Aidha, Rais Magufuli alisema serikali yake inaendelea kuijenga Tanzania mpya kwa kuhakikisha inaondoa kila kilicho kichafu na kuziba mianya ya rushwa.

UNUNUZI WA MELI, VIWANJA VYA NDEGE
Akizungumzia moja ya mafanikio jana, Rais Magufuli alisema tayari katika kipindi chake cha miezi 23, serikali imetengeneza meli mbili za MV Iringa na Mv Ruvuma ambazo zinatoa huduma katika
Ziwa Nyasa.

Pia alisema serikali inakamilisha ukarabati wa Mv Victoria na MV Butiama, huku pia ipanua Bandari ya Tanga ambayo imetengewa Sh. bilioni 16 kwa ajili ya kufanyiwa ukarabati.

Aidha, mbali na kununua ndege mbili za bombardier kwa ATCL na zingine nne zikitarajiwa kutua mwakani, serikali pia imeshaanza taratibu za kukamilisha upanuzi wa viwanja vikubwa vya ndege na kwamba nchi haiwezi kununua ndege endapo hakuna viwanja vya kisasa.

Alisema Sh. bilioni 560 zinatumika kupanua viwanja vya ndege vya kimataifa vya Julius Nyerere pamoja na Kilimanjario (Kia) ambao umepanuliwa kwa Sh. bilioni 91. Pia alisema ukarabati wa viwanja vingine 11 vya ndege uanendelea, vikiwamo vya Mwanza (Sh. bilioni 90), Mtwara Sh. bilioni 46, Shinyanga Sh. bilioni 49.2, Sumbawanga Sh. bilioni 55.9, Musoma Sh. bilioni 21, Songea Sh. bilioni 21 na Iringa Sh. bilioni 39.

BARABARA, FLY-OVERS, UMEME
Rais Magufuli alisema katika miezi 23, serikali imejenga barabara mpya za lami zenye urefu wa kilomita 1,500, zikiwa na thamani ya  Sh. trilioni 1.8. Pia alitaja kuwapo kwa ujenzi wa barabara za juu unaoendelea katika miradi ya Tazara ambao umetengewa Sh. bilioni 94.03 na Ubungo ambao utatumia Sh. bilioni 177.42.

Kuhusu umeme, alisema wamefanikisha pia ujenzi wa mradi wa Kinyerezi I kwa dola za Marekani milioni 344  na Kinyerezi II dola 188 na jumla ya triloni 1.2 zitahitajika kukamilisha mradi huo ukikamilika utazalisha umeme wa megawati 565 kwa kutumia gesi ya asili. Pia alisema maandalizi ya mradi wa  Kinyerezi III yanaendelea.

Aidha, alitaja mafanikio pia katika miradi ya umeme vijini inayotekelezwa na Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kwa mradi wa awamu ya tatu (REA III) kwa kuhusisha zaidi ya vijiji  400 kwa gharama ya Sh. bilioni 587 umepangwa kufanyika mwaka huu. Tayari pia wameanza awamu ya tatu kwenye vijiji 7,873.

WATUMISHI HEWA, VYETI FEKI
Rais Magufuli alisema kuwa hadi sasa, serikali imeondoa watumishi hewa 20,000 ambao walikuwa wakiigharimu serikali Sh. bilioni 19.848 kwa mwezi na kwa mwaka kuwa Sh. bilioni 238.176.

Pia alisema wameondoa pia watumishi wenye vyeti feki 12,000 ambao walikuwa wakilipwa Sh. bilioni 11.9008 kwa mwezi na bilioni 142.9 kwa mwaka, na kwamba kwa ujumla, Sh. bilioni 381 zilikuwa zikilipwa kwa watumishi hewa na wenye vyeti feki.

Aidha, Rais Magufuli alisema kuwa serikali imefuta utitiri wa kodi zilizokuwa kero, zikiwamo tozo 80 kwa wakulima, saba kwa wafugaji, na wavuvi tozo tano na kufuta ushuru kwa mazao yanayosafirishwa kutoka halmashauri moja hadi nyingine yakiwa na uzito usiozidi tani moja. Pia serikali imefanikisha kupunguza bei ya mbolea.

UKUAJI UCHUMI, UDHIBITI MADINI
Alisema uchumi unakuwa kwa asilimia 7.1 na kuifanya Tanzania kuwa moja ya nchi zinazofanikiwa katika eneo hilo Afrika, ikitanguliwa na Ethiopia yenye ukuaji wa asilimia 8.3 na kwamba ukuaji wake unaenda sambamba na India.

Pia alisema Tanzania imekuwa ikivutia zaidi wawekezaji, hiyo ikiwa ni kwa mujibu wa ripoti za taasisi mbalimbali ikiwamo AfDB na UNDP. Pia mfumuko wa bei umedhibitiwa na kuwa asilimia tano.

Aidha, Rais Magufuli alizungumzia pia mafanikio katika vita inayoendelea ya uchumi ambapo hadi sasa, serikali inaendelea kudhibiti upotevu wa mapato kupitia uchimbaji wa madini ya dhahabu, almasi na tanzanite.

Rais alisema Tanzania ilikuwa ikiambulia asilimia tano tu ya mauzo ya tanzanite duniani licha ya kwamba madini hayo hayapatikani kwingine zaidi ya Tanzania.

Allitaja mafanikio kuwa hadi sasa, katika kipindi kifupi cha udhibiti, uzalishaji wa Tanzanite umeongezeka mara 30 na kwamba siku moja walifanikiwa kuzalisha kilo zaidi ya 18, jambo ambalo halijawahi kutokea tangu kuanza uchimbaji wa madini hayo.

“Tulipozuia kidogo, katika siku chache, production (uzalishaji) ya tanzanite imekuwa zaidi ya mara 30… kuna siku moja wamepata kilo 18, haijawahi kutokea tangu tanzanite ianze kuchimbwa,” alisema Rais Magufuli.

VITA DHIDI YA RUSHWA, UFISADI
Alisema serikali inaendelea na mapambano dhidi ya rushwa na ufisadi katika kila sekta, ikiwamo katika benki ambazo baadhi zilikuwa zikitumia kupitishia fedha za rushwa.

Rais Magufuli alisema vilevile kuwa wizi kupitia ruzuku ya pembejeo za kilimo unaendelea kudhibitiwa na hadi sasa, imebainikia katika halmashauri 140 zilizokaguliwa kuwa pembejo hewa zilizopitishwa ni za thamani zaidi ya Sh. bilioni 57.9, huku wahusika wakiandikisha hadi waliofariki.

Alisema vilevile kuwa katika kipindi cha miezi 23, serikali imedhibiti matumizi holela yakiwa ya safari za nje na ndiyo maana baadhi ya watu waliokuwa wakinufaika kwa fedha za burebure wamekuwa wakilalamika kuwa fedha hazionekani mitaani.

“Mtu anayesafiri nje kila wiki, hawezi kufurahia hatua tunazochukua,” alisema Rais Magufuli.

UDHIBITI KAYA HEWA, WANAFUNZI HEWA
Alisema zimebainika kuwapo kaya hewa 57,000 ambazo ziliandikishwa na kunufaika kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (Tasaf) na sasa, serikali yake imedhibiti upotevu huo na kuchukua hatua.

Pia jumla ya wanafunzi hewa 65,000 kutoka shule za msingi na sekondari walibainika na sasa fedha zake zimeokolewa huku hatua zikichukuliwa dhidi ya wahusika. Hali kama hiyom ilikuwapo pia katika utoaji wa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu ambako ilibainika kuwa mikopo 8,500 ilikuwa ni ya wanafunzi hewa.

Aidha, Rais Magufuli alizungumzia mafanikio katika vita dhidi ya dawa za kulevya, utoaji wa elimu bure kwa kufuta ada na kupeleka ruzuku shuleni na pia kuhamia Dodoma ambapo makamu wa Rais atahamia mkoani humo mwishoni mwa mwaka huu na yeye atahamia mwakani.

Alisema kuwa hadi sasa, watumishi zaidi ya 3,000 wamehamia pamoja na mawaziri wakiongozwa na Waziri Mkuu.
ads
Bonyeza HAPA kudownload applicationi ya SWAHILI NEWS kwenye simu yako ili kupata habari zetu Haraka
Share To:

SWAHIBA MEDIA STAFF

Habari , karibu katika mtandao wetu ili kuhabarika na stori zote za siku katika lugha yetu adhwim ya kiswahili, habarika wakati wote weka dunia kiganjani mwako na swahili news

Post A Comment: