WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amesema jumla ya kampuni 25 zimeonesha nia ya kujenga viwanda vya uchenjuaji makinikia nchini.
Majaliwa alitoa kauli hiyo jana alipokuwa akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi(CCM) ya mwaka 2015 hadi 2020 kwa kipindi cha miaka miwili katika mkutano mkuu wa tisa wa chama hicho, mjini hapa.
Alisema serikali imehamasisha wawekezaji wa mitambo ya uchenjuaji kujitokeza kwa ajili ya kujenga viwanda hivyo hapa nchini.
“Jumla ya kampuni 25 zimeonesha nia," alisema Majaliwa na kwamba "Serikali inaendelea na utaratibu wa kutafuta kampuni zitakazofaa kwa ajili ya ujenzi wa mitambo hiyo".
"Vilevile, Serikali itaendelea kuisimamia na kuilinda sekta ya madini na itaendelea kujiridhisha kuwa Watanzania wananufaika vizuri.”
Rais Magufuli alipiga marufuku usafirishaji wa mchanga wa madini nje ya nchi na kutaka ufanyiwe uyeyushaji hapa hapa nchini Machi 2, mwaka huu wakati akiweka jiwe la msingi la kiwanda cha kutengeneza vigae cha Goodwill, kilichopo wilaya ya Mkuranga mkoani Pwani.
Akizungumza baada ya kutembelea kiwanda hicho, Rais Magufuli aliishukuru menejimenti ya kiwanda hicho kwa uwekezaji huo na kuelezea kufurahishwa kwake na kutumika kwa teknolojia ya kuyeyusha mchanga wa kutengenezea vigae.
"Nchi hii tumechezewa vya kutosha, sasa nyinyi hapa mnayeyusha mchanga kwa kuuchemsha hadi nyuzi joto 1,000 wakati wengine (wenye migodi) wanasafirisha mchanga nje ya nchi wakati uchemshaji wake hauhitaji kufika hata nyuzi joto 1,000," alisema Rais Magufuli siku hiyo.
"Naiagiza Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji na Wizara ya Nishati na Madini kuwa kuanzia sasa ni marufuku kusafirisha mchanga nje ya nchi." Alisema zaidi Rais Magufuli, lakini wiki tatu baadaye akagundua makontena 20 ya bidhaa hiyo ya kampuni ya Acacia yakisubiri kupandishwa meli baada ya kufanya ziara ya kushtukiza kwenye Bandari ya Dar es Salaam.
Tangu hapo ilikuja kugundulika kuwa kuna jumla ya makontena 276 yaliyokuwa kwenye Bandari ya Dar es Salaam na bandari kavu ya Mofed, na kamati mbili zilizoundwa na Rais Magufuli kuchunguza kilichomo ilibaini udanganyifu mkubwa.
Kwa mujibu wa kamati maalumu ya kuchunguza masuala ya kisheria na kiuchumi kuhusiana na makinikia yanayosafirishwa nje ya nchi iliyowasilishwa Ikulu jijini Dar es Salaam Juni 12, mwaka huu nchi inaweza kuwa imepoteza mpaka Sh. trilioni 489 katika miaka 19 iliyopita.
Kamati hiyo iliundwa na Rais Magufuli Aprili 10 ikiwa na wajumbe nane wabobezi katika sheria na uchumi, na mwenyekiti wake Profesa Nehemia Osoro ilisema kwa kima cha chini, nchi imepoteza Sh. trilioni 252 katika kodi na thamani ya madini yaliyotoroshwa kupitia makinikia.
SERA MADHUBUTIAidha, Majaliwa alisema kwa kipindi cha miaka miwili tangu uchaguzi mkuu wa 2015, Serikali imeendelea kutekeleza changamoto zinazowakabili wananchi kwa kuweka sera madhubuti zinazosaidia kutatua changamoto mbalimbali.
Kadhalika, alisema serikali inaimarisha ukaguzi wa uzalishaji na mauzo ya madini katika migodi mikubwa na midogo nchini ambapo katika kipindi cha Novemba, 2015 hadi mwezi uliopita, jumla ya sampuli 8,497 za dhahabu na makinikia ya shaba kutoka kwenye migodi mikubwa zilifanyiwa uchunguzi kwenye maabara ili kujua kiasi na thamani ya madini yaliyozalishwa na kuuzwa nje.
Aidha, Majaliwa alisema kaguzi pia zilifanywa katika migodi ya Tanzanite One na Mgodi wa Makaa ya Mawe wa Ngaka ambazo zimeiwezesha Serikali kukusanya mrabaha wa jumla ya Dola za Marekani milioni 6.99.
Majaliwa alisema serikali iliweka dhamira ya kuwahudumia wananchi wote, hususan maskini kwa kuwapelekea miradi ya maendeleo na huduma muhimu za jamii.
“Ili kufikia azma hii ilibidi tuanze kujenga nidhamu ya watumishi wa umma kwa kubaini wazembe, wabadhirifu, wezi wa mali na fedha za umma, wala rushwa mahali pa kazi na wasio tayari kuwatumikia wananchi na hasa wanyonge,” alisema Majaliwa.
Alisema walianzisha mapambano ya wazi dhidi ya vitendo vya rushwa na ufisadi pamoja na mapambano dhidi ya matumizi ya dawa za kulevya.
Kuhusu utalii, Majaliwa alisema serikali imeendelea kuboresha miundombinu yake ikiwamo ukarabati wa kilometa 2,571 za barabara zilizopo ndani ya hifadhi, njia za miguu zenye urefu wa kilometa 143.5 na kuongeza matangazo ya utalii ndani na nje ya nchi.
“Juhudi hizo zimewezesha idadi ya watalii kuongezeka kutoka 1,137,182 mwaka 2015 hadi 1,284,279 mwaka 2016, sawa na ongezeko la asilimia 12 na kuliingizia taifa dola za Marekani bilioni 2," alisema.
“Aidha, katika mwaka wa fedha 2017/2018 Serikali imeongeza bajeti ya utalii hadi kufikia Sh. bilioni 6.6 ikilinganishwa na Sh. bilioni 4.2 zilizotengwa mwaka 2016/2017.”
Post A Comment: