BEKI wa zamani wa Arsenal, Martin Keown amesema anaamini sasa siku za Arsene Wenger zimeanza kuhesabika.
Kauli ya Keown, ambaye anaonekana kuwa na mapenzi makubwa na Arsenal, imekuja baada ya timu hiyo kushuka hadi nafasi ya saba katika msimamo wa Ligi Kuu England baada ya sare ya bila kufungana dhidi ya West Ham United juzi Jumatano. Arsenal sasa imecheza mechi tatu bila ya kuambulia ushindi, imepigwa moja na kutoa sare mbili.
Sambamba na hilo, Arsenal wameonekana kuwa dhaifu sana kwenye mechi zao za ugenini baada ya kukusanya pointi tisa tu katika mechi tisa, ikiwa ni mwendo mbovu zaidi katika historia yake kwenye Ligi Kuu England.
Keown, ambaye alidumu kwenye timu hiyo ya Arsenal kwa miaka 13 katika zama mbili tofauti alisema anachokiona kwa sasa ni Wenger siku zake kuelekea ukingoni katika kuwa kocha wa timu hiyo licha ya kusaini mkataba wa miaka miwili hadi mwaka 2019.
"Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa sasa kinaonekana si kitu kinachoweza kutokea kwa Arsene Wenger na maswali yataanza kuibuka tena kuhusiana na kocha, kwamba nani atakuja kuchukua nafasi," alisema Keown.
"Kama atashindwa kufanya vizuri, basi mwisho wa msimu ni heri afunge tu mikono yake na kusema: 'Pengine mimi si mtu sahihi kwa sasa kuipeleka timu hii mbele.’"
Arsenal ilishindwa kufuzu kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya na hivyo msimu huu inacheza kwenye Europa League ambapo ilifanikiwa kuingoza kundi lake na kufanikiwa kutinga kwenye hatua ya 32 bora.
Post A Comment: