MFANYAKAZI wa Mgodi wa Geita (GGM), Milembe Suleiman, anashikiliwa na Jeshi la Polisi mkoani Geita kutokana na kujihusisha na mapenzi ya jinsia moja.


Awali, picha za video za mtuhumiwa huyo zilisambaa kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii , zikimuonyesha akiwa na anayedaiwa kuwa mpenzi wake katika tukio linaloelezewa kuwa ni la kuvishana pete ya uchumba baina ya wawili hao.

 Mijadala mbalimbali ya kuwalaani wawili hao ilipamba moto kwenye mitandao ya kijamii, hasa facebook na kwenye makundi mbalimbali ya whatsapp, binti mrembo anayedaiwa kuwa ndiye mke mtarajiwa wa mtuhumiwa akidaiwa kuwa ndugu wa mmoja wa naibu mawaziri wa serikali ya sasa ya awamu ya tano.

Wawili hao wanaonekana kwenye picha za video wakikumbatiana, kubusiana, kunyonyana ndimi kama wapenzi na pia ‘biharusi’ mtarajiwa akionyesha kwa madaha kidole chake chenye pete huku wakishangiliwa mara kadhaa na watu waliokuwa nao kwenye eneo la tukio lililokuwa na meza iliyojaa vinywaji na ‘makulaji’.

 Hata hivyo, Nipashe haikupata uthibitisho kutoka kwenye chanzo huru kuhusiana na ukweli juu ya uhusiano wa binti huyo na naibu waziri.

 Akizungumza na Nipashe jana, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Mponjoli Mwabulambo, alisema kuwa wanamshikilia Milembe , ambaye ni Ofisa Ugavi Kitengo cha Manunuzi wa GGM, kwa uchunguzi kabla ya kuchukuliwa kwa hatua zaidi za kisheria kwakuwa vitendo vya mapenzi ya jinsia moja haviruhusiwi nchini.

Alipoulizwa juu ya suala hilo jana, Makamu wa Rais wa GGM anayeshughulikia uendeshaji, Simon Shayo, alikiri kuwa Milembe ni mfanyakazi wa mgodi huo.

Hata hivyo, Shayo alisema kwakuwa jambo hilo linashughulikiwa na polisi, hawawezi kulizungumzia kwa sasa.

 “Amekamatwa kwa makosa hayo. Tunasubiri polisi wafanye kazi zao… hatuwezi kuingilia kwa sababu makosa hayo hakuyatenda akiwa kazini. Alikuwa uraiani, kampuni haihusiki na vitendo vya mtu akiwa mtaani,” alisema Shayo.


ads
Bonyeza HAPA kudownload applicationi ya SWAHILI NEWS kwenye simu yako ili kupata habari zetu Haraka
Share To:

SWAHIBA MEDIA STAFF

Habari , karibu katika mtandao wetu ili kuhabarika na stori zote za siku katika lugha yetu adhwim ya kiswahili, habarika wakati wote weka dunia kiganjani mwako na swahili news

Post A Comment: