SIMBA sasa washindwe wenyewe iwapo wanahitaji huduma ya mshambuliaji wa Nkana FC ya Zambia, Walter Bwalya, baada ya mchezaji huyo kuweka wazi kuwa yupo tayari kutua Msimbazi iwapo pande hizo mbili zitafikia makubaliano.

Benchi la ufundi la Simba linaloongozwa na Mcameroon Joseph Omog, wamependekeza kutafutiwa mshambuliaji mwenye uwezo wa hali ya juu, huku wakilitaja jina la Bwalya na tayari jukumu la kumfikisha mshambuliaji huyo Msimbazi, ametwishwa Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya klabu hiyo, Zacharia Hans Poppe.

Kigogo mmoja mwenye ushawishi mkubwa ndani ya Simba, ameliambia gazeti la BINGWA  kuwa dau la Bwalya litakuwa kubwa, lakini Kamati ya Usajili chini ya Poppe itafanya kila linalowezekana wazungumze naye kwani wana uwezo wa kujichangisha kupata fedha atakazozihitaji.

β€œUnajua yule jamaa (Bwalya) kama unakumbuka misimu kadhaa, tulitaka kumsajili, lakini dau lake likawa kubwa sana, tukamshindwa lakini sasa tumeona tufanye kila linalowezekana tumchukue,” alisema.

Wakati Simba wakiendelea na mchakato huo, tayari mmoja wa viongozi wa Azam anatarajia kutua Zambia kumalizana na mchezaji huyo ili kuja kuziba pengo la mshambuliaji wao wa zamani, Kipre Tchetche.

Azam wanaonekana kupania kumnasa Bwalya kwani ni miongoni mwa mapendekezo ya kocha wao, Aristica Cioaba, wakiwa wamelenga kukiboresha kikosi chao kiweze kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara unaowaniwa pia na mabingwa watetezi, Yanga pamoja na Simba.

β€œSi Simba pekee, niko tayari kucheza timu yoyote ile itakayokuja na ofa nzuri na kuridhika nayo,” alisema Bwalya.

Bwalya ambaye uraia wake una utata kutokana na kudaiwa kuwa ni Mkongo, huku pia akihusishwa na uraia wa Zambia, ni mmoja wa mastraika wenye uwezo mkubwa wa kucheka na nyavu na kama timu mojawapo kati ya Simba au Azam itafanikiwa kuinasa saini yake, itakuwa imelamba dume.
ads
Bonyeza HAPA kudownload applicationi ya SWAHILI NEWS kwenye simu yako ili kupata habari zetu Haraka
Share To:

SWAHIBA MEDIA STAFF

Habari , karibu katika mtandao wetu ili kuhabarika na stori zote za siku katika lugha yetu adhwim ya kiswahili, habarika wakati wote weka dunia kiganjani mwako na swahili news

Post A Comment: