WAKATI dirisha dogo la usajili likifunguliwa leo, baadhi ya nyota wa kimataifa kwenye klabu kongwe za Simba na Yanga zinazodhaminiwa na Kampuni ya Kubashiri Matokeo Michezoni ya SportPesa, wamekalia kuti kavu na huenda wakaonyeshwa mlango wa kutokea.


Mbali na nyota wa kigeni, lakini pia wamo wachezaji wazawa ndani ya klabu hizo ambao wapo kwenye hatihati ya kutupiwa virago kutokana na sababu mbalimbali.

Moja ya sababu zinazotajwa ni pamoja na kushuka kwa viwango pamoja na kuwa majeruhi kwa muda mrefu.

Kapombe, Gyan, Mavugo

Ndani ya kikosi cha Simba beki Shomari Kapombe ni miongoni mwa wachezaji wazawa ambao wanaweza wakatupiwa virago kwenye dirisha hili.

Majeraha yaliyomuweka nje kwa muda mrefu yanamuweka katika hatari ya kufunguliwa mlango wa kutokea ndani ya kikosi hicho.

Tangu asajiliwe na Simba katika dirisha kubwa la usajili lililopita akitokea Azam, Kapombe hajaichezea Simba mchezo wowote wa Ligi Kuu msimu huu.

Aidha, kitendo cha Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya klabu hiyo kueleza hadharani kuwa nyota huyo amepona, lakini amekuwa muoga kurejea uwanjani kinatoa picha ya mwisho wa mchezaji huyo ndani ya Simba.

Kwa upande wa Laudit Mavugo na Nicolaus Gyan, wenyewe wapo hatihati ya kutemwa kutokana na kushindwa kuonyesha kiwango kilichotarajiwa.

Nyota hao licha ya kupata nafasi kwenye kikosi cha kocha Joseph Omog katika mechi za Ligi Kuu, bado wameshindwa kuonyesha kitu cha ziada.

Kwa upande wa mabingwa watetezi, Yanga, mshambuliaji Donald Ngoma naye anaweza akapewa mkono wa kwaheri.

Ngoma licha ya kutopewa ruhusa na uongozi wa timu hiyo, ameondoka nchini kwenda kwao Zimbabwe kwa kile alichokielezea kwenda kujitibia majeraha yake ya mguu.

Hata hivyo, Katibu Mkuu wa klabu hiyo, Boniface Mkwasa, akinukuliwa wiki iliyopita, alisema Ngoma alitakiwa kuwasiliana na kocha na meneja wa timu kabla ya kuondoka kwake.

β€œNilimwambia arudi kwa kocha na meneja kuomba ruhusa kabla ya kufika ofisini kwangu, lakini hakurudi tena kwangu,” alisema Mkwasa.

Aidha, kitendo cha kuwa nje kwa muda mrefu na kushuka kwa kiwango chake kutokana na majeraha kinaweza kikamfungulia mlango wa kutokea nyota huyo.

Dirisha dogo la usajili lililofunguliwa leo litafungwa Desemba 15, mwaka huu.
ads
Bonyeza HAPA kudownload applicationi ya SWAHILI NEWS kwenye simu yako ili kupata habari zetu Haraka
Share To:

SWAHIBA MEDIA STAFF

Habari , karibu katika mtandao wetu ili kuhabarika na stori zote za siku katika lugha yetu adhwim ya kiswahili, habarika wakati wote weka dunia kiganjani mwako na swahili news

Post A Comment: