MATAJIRI wa Yanga waliopo katika Kamati ya Usajili na ile ya Utendaji, wanatarajia kukutana na benchi la ufundi la timu hiyo kujadili namna gani wanavyoweza kukabiliana na wapinzani wao wa jadi Simba katika suala zima la usajili, lakini pia kampeni yao ya kutetea ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL).


Hilo limekuja baada ya kubaini iwapo hawatakuwa makini, wanaweza kujikuta wakipoteza ubingwa wao wa Bara wanaoushikilia kwa msimu wa nne sasa, baada ya mfanyabiashara maarufu nchini, Mohammed Dewji ‘Mo’, kuonyesha nia ya kuipa mafanikio makubwa Simba.

Hivi karibuni, Mo Dewji alitangazwa kama mshindi wa zabuni ya uwekezaji wa asilimia 49 katika klabu ya Simba na kwamba, tayari mdau huyo wa soka ametangaza kuifanyia makubwa klabu hiyo kuanzia kwenye usajili wa wachezaji, ujenzi wa viwanja na uwekezaji kwa ujumla.

Kwa kufahamu hilo, vibopa wa Yanga wameona hawana budi kukutana ili kuona ni vipi wanaweza kukabiliana na Mo, lakini pia kuweka mikakati kabambe itakayowahakikishia kutetea ubingwa wao na kwamba yeyote ndani yao atakayekwenda kinyume nao, hawatakuwa tayari kumfumbia macho.

Habari kutoka ndani ya Yanga zinasema kuwa jambo la kwanza ambalo vibopa hao pamoja na viongozi wa benchi la ufundi watalifanyia kazi, ni kuharakisha usajili wa straika hatari wa nchini Benin, Marcen Koukpo anayechezea klabu ya Bufalo FC ya huko.

Chanzo chetu cha uhakika kimedokeza kuwa kwa kufahamu kwamba dirisha dogo la usajili linafungwa Desemba 15, mwaka huu, huku ligi ya Benin ikifikia tamati Desemba 25, vibopa hao wanataka kuangalia ni namna gani wanaweza kuipata saini ya Koukpo katika kufungwa kwa dirisha la usajili huo.

Alisema Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Yanga, Hussein Nyika, amerejea nchini na jina la straika huyo lakini tatizo mazungumzo kati ya Yanga na Buffalo, hayajafikia mwafaka hivyo kikao hicho ndicho kitaamua mustakabali wa kumsajili nyota huyo kama anaweza kuja kusaini kabla ya dirisha dogo la usajili kufungwa kisha kurejea katika timu yake kuendelea na majukumu hadi Januari ndio atue rasmi Jangwani.

“Tumetakiwa kusubiri hadi Desemba 25 ligi ya Benin itakapomalizika ndio tuone uwezekano wa kumsajili huyo Marcen, lakini kumbuka dirisha la usajili mdogo linafungwa Desemba 15, hivyo hapo kunatakiwa kufanyika jambo la ziada ndio maana viongozi wetu wa kamati wameamua kukutana ili kuona nini cha kufanya,” alisema mtoa habari wetu huyo.

Yanga imeamua kutupa ndoana kwa Koukpo baada ya kuwasajili wachezaji wawili ambao ni Mkongoman Piston Kayembe na Yohana Mkomola wa Serengeti Boys, huku pia ikiwapigia hesabu Walter Bwalya wa Nkana ya Zambia na Yusuph Ndikumana ambaye inadaiwa dili baina ya pande hizo mbili linaelekea ukingoni.

Kocha Mkuu wa Yanga, George Lwandamina, anataka kuongeza nguvu katika kikosi chake ambacho kinatarajia kuwa na kazi ya ziada kutetea ubingwa wao wa VPL, lakini pia ushiriki wao katika michuano ya Ligi Mabingwa Afrika mwakani.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Yanga, Charles Mkwasa, alisema kuwa azma yao ni kuhakikisha wanatetea ubingwa wao wa Bara kwa gharama yoyote ile, ikiwamo kufanya kweli kwenye kipute cha Ligi ya Mabingwa Afrika mwakani.

“Dhamira yetu ipo wazi, tuweze kutetea ubingwa wetu wa VPL kwa mara ya tano mfululizo, lakini pia kufika mbali kwenye michuano ya kimataifa hapo mwakani, tukiamini tunao uwezo wa kufanya hivyo kutokana na ubora wa kikosi chetu, benchi la ufundi na mikakati ya kamati zetu na uongozi na klabu kwa ujumla,” alisema.

Credit - Bingwa
ads
Bonyeza HAPA kudownload applicationi ya SWAHILI NEWS kwenye simu yako ili kupata habari zetu Haraka
Share To:

SWAHIBA MEDIA STAFF

Habari , karibu katika mtandao wetu ili kuhabarika na stori zote za siku katika lugha yetu adhwim ya kiswahili, habarika wakati wote weka dunia kiganjani mwako na swahili news

Post A Comment: