KOCHA wa Lipuli FC, Selemani Matola, amesema amekiandaa vyema kikosi chake kuhakikisha kinaondoka na ushindi katika mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Simba, ambayo itafanyika Jumapili kwenye Uwanja wa Chamazi jijini Dar es Salaam na kutahadharisha hakuna "mbeleko".


Akizungumza na gazeti la Nipashe kwa njia ya simu jana akiwa Iringa, Matola, alisema kuwa anafahamu wazi mechi hiyo itakuwa ngumu kama alivyocheza dhidi ya mabingwa watetezi Yanga kwa sababu inaundwa na wachezaji wengi wenye uzoefu.

Matola alisema kuwa licha ya uzoefu huo, amewaandaa wachezaji wake kukabiliana na changamoto watakazokutana nazo uwanjani ili kuhakikisha hawapotezi mchezo huo.

"Ni mechi inayotazamwa kwa macho mengi, lakini kwa upande wetu tumejipanga kama tunavyojipanga katika mechi nyingine, tunajua ukishinda unapata pointi zote na ukitoa sare mnagawana, tumedhamiria kuendeleza rekodi nzuri tunapocheza Dar es Salaam," alisema nahodha na kiungo huyo wa zamani wa Wekundu wa Msimbazi.

Aliongeza kuwa wachezaji wake wote ni wazima na wanatarajia kuwasili Dar es Salaam kesho tayari kuwavaa vinara hao wanaodhaminiwa na Kampuni ya Kubahatisha Matokeo Michezoni ya SportPesa.

Katika msimamo wa ligi, Lipuli FC ambayo imepanda daraja msimu huu pamoja na Singida United na Njombe Mji, iko katika nafasi ya saba ikiwa na pointi 13 baada ya kushinda mechi tatu na kutoka sare michezo minne.
ads
Bonyeza HAPA kudownload applicationi ya SWAHILI NEWS kwenye simu yako ili kupata habari zetu Haraka
Share To:

SWAHIBA MEDIA STAFF

Habari , karibu katika mtandao wetu ili kuhabarika na stori zote za siku katika lugha yetu adhwim ya kiswahili, habarika wakati wote weka dunia kiganjani mwako na swahili news

Post A Comment: