TIMU za soka za Taifa za Zimbabwe na Libya zinatarajia kushiriki katika mashindano ya kuwania ubingwa wa Kombe la Chalenji yatakayofanyika kuanzia Novemba 25 hadi Desemba 9 mwaka huu jijini Nairobi, Kenya imeelezwa.


Katibu Mkuu wa Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA), Nicholas Musonye, alisema jana nchi hizo zimetuma barua ya kukubali mwaliko wa kuwa timu mwalikwa ambazo anaamini zitasaidia kuongeza ushindani kwenye michuano hiyo ambayo mwaka jana haikufanyika.

"Tunapenda kutoa shukrani kwa wote ambao wanashirikiana na CECAFA katika kuendeleza soka la ukanda huu, pia tunapenda kuwajulisha kuwa baada ya kusaini makubaliano rasmi ya kuongeza umoja kati ya CECAFA, COSAFA na Kanda ya Kaskazini (UNAF), tunapenda kuwafahamisha kuwa Zimbabwe na Libya zimethibitisha kushiriki mashindano ya Kombe la Chalenji mwaka huu," alisema Musonye.

Alisema kuwa mpaka sasa ni nchi 12 zimeshathibitisha kushiriki michuano hiyo ambayo ni pamoja na wenyeji Kenya, Uganda, Tanzania Bara, Rwanda, Burundi, Sudan, Sudan Kusini, Ethiopia, Zanzibar, Somalia, Zimbabwe na Libya.

Aliongeza kuwa kabla ya kuanza kwa michuano hiyo, wanachama wa baraza hilo wanashiriki katika mkutano mkuu wa mwaka ambao utajadili mambo mbalimbali ya maendeleo ya ukanda huo.

Tayari CECAFA ilishatangaza kuwa Rwanda itakuwa mwenyeji wa mashindano ya Kombe la Chalenji kwa Wanawake yatayofanyika Novemba 3 hadi 12 mwaka huu na Burundi itakuwa mwenyeji wa michuano ya vijana wa umri chini ya miaka 17 hapo mwakani.
ads
Bonyeza HAPA kudownload applicationi ya SWAHILI NEWS kwenye simu yako ili kupata habari zetu Haraka
Share To:

SWAHIBA MEDIA STAFF

Habari , karibu katika mtandao wetu ili kuhabarika na stori zote za siku katika lugha yetu adhwim ya kiswahili, habarika wakati wote weka dunia kiganjani mwako na swahili news

Post A Comment: