SERIKALI imewaondoa hofu wakazi wa Jiji la Dar es Salaam kwamba hakutakuwa na msongamano wa magari eneo la Ubungo wakati ujenzi wa barabara za juu (fly over) utakapokuwa unaendelea.


Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi  na Mawasiliano,  Profesa Makame Mbarawa, aliyasema hayo wakati akizungumza na gazeti la  Nipashe lililotaka kufahamu namna gani serikali itapambana na foleni wakati ujenzi wa 'fly over' utakapoanza.

" Tumejipanga,  kutakuwa na njia za pembeni kuhakikisha magari yanapita wakati ujenzi unaendelea.  Hakutakuwa na foleni,  wananchi wasiwe na wasiwasi, " alisema Waziri Mbarawa.

Alisema kwa sasa mjenzi wa mradi huo kwa kushirikiana na Wakala wa Barabara (Tanroads) mkoa wa Dar es Salaam, wameshaanza kubuni njia za pembeni zitakazotumiwa pia na watembea kwa miguu.

Waziri Mbarawa alisema licha ya serikali kuweka mikakati katika eneo hilo la Ubungo, pia ujenzi wa barabara za kupunguza msongamano katika Jiji la Dar es Salaam ziko katika hatua za mwisho kukamilika.

Alisema barabara ya Goba-Makongo (Km 4.5) imekamilika kwa asilimia 52, Goba-Madale (kilomita tano) ikiendelea na ujenzi, barabara ya Kimara Baruti-Msewe (Km 2.6) imekamilika kwa asilimia 80 na ile ya Kifuru-Msigani (Km 4.5) ikiwa imekamilika kwa asilimia 87.

"Serikali ilikuwa na mpango wa kupunguza msongamano katika Jiji la Dar es Salaam tangu mwaka 2008. Tulikuwa na awamu tatu, awamu ya tatu ilianza Desemba mwaka jana na ilihusu barabara tatu zenye urefu wa kilomita 14, zilizogharimu Sh. bilioni 24.2," alisema.

Alisema barabara hizo zitakapokamilika zitapunguza msongamano katika Jiji la Dar es Salaam kwa asilimia kubwa  na kwamba wananchi watoe ushirikiano ili miradi hiyo ikamilike kwa wakati.

Naye Tanroads  Mkoa wa Dar es Salaam,  Julius Ndyamkama, alisema gharama za mradi wa barabara ya Kifuru-Msigani ni Sh. bilioni 8.4 na inatarajiwa kukamilika Desemba 6, mwaka huu. Mkandarasi anayejenga ni Kampuni ya Estim Comstruction Co. Ltd na ameshalipwa Sh. bilioni nne.

Alisema barabara ya Goba-Makongo inayofadhiliwa na Serikali ya Tanzania gharama za ujenzi ni Sh. bilioni 7.73 na itakamilika Januari 30, mwakani.

"Kuna changamoto kwani baadhi ya maeneo yana nyumba ambazo zinahitaji kufidiwa,  hivyo kazi za ujenzi haziendi kama inayotarajiwa, hasa kipande cha barabara kuanzia Mto Mbezi kwenda Makongo," alisema Ndyamkama.

Ndyamkama alisema gharama za mradi wa barabara ya Goba -Madale unaofadhiliwa na Serikali ya Tanzaniani Sh. bilioni 8.06 na unatarajiwa kukamilika Septemba 30, mwakani
ads
Bonyeza HAPA kudownload applicationi ya SWAHILI NEWS kwenye simu yako ili kupata habari zetu Haraka
Share To:

SWAHIBA MEDIA STAFF

Habari , karibu katika mtandao wetu ili kuhabarika na stori zote za siku katika lugha yetu adhwim ya kiswahili, habarika wakati wote weka dunia kiganjani mwako na swahili news

Post A Comment: