MKUU wa Jeshi la Polisi nchini, Inspekta Jenerali (IGP) Simon Sirro, amewajia juu baadhi ya wanasiasa wanaotaka kuharakishwa kwa uchunguzi wa shambulizi dhidi ya Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu.


IGP Sirro amesema wanasiasa wanapaswa kuendelea kufanya siasa na jeshi lifanye kazi yake na waache kushinikiza masuala ambayo hayawahusu kama vile uchunguzi wa suala hilo.

Sirro alisema hayo jana wakati akizungumza na waandishi wa habari mkoani Njombe, akiwa kwenye ziara ya kikazi ya siku moja mkoani hapa.

Alisema jeshi hilo linaendelea na uchunguzi wa tukio hilo na litatoa taarifa juu ya hatua waliyofikia kwa kuwa jarada la tukio hilo bado wanalo na wanasiasa hawawezi kuwafundisha watu wa kuwahoji.

Aidha, Sirro alisema wanasiasa wanazungumza ili waonekane kwa wapigakura wao na wanakula posho kwa kuzungumza, hivyo hawezi kuwazuia kufanya hivyo.

Pia alisema wanasiasa wanafanya siasa kwa kuwa kuna amani, hivyo wamwache aendelee kufanya kazi yake ya kuhakikisha Watanzania wanakuwa na amani na kwamba tunu hiyo ikitoweka wanasiasa hawatafanya siasa.

Juzi, familia ya Lissu ilizungumza na waandishi wa habari ikilitaka Jeshi la Polisi liharakishe uchunguzi wa suala hilo kwa madai kuwa ni siku nyingi zimeshapita lakini hakuna kinachoendelea.

Jana, Chadema ilifanya mkutano na waandishi wa habari na kuhoji jeshi hilo kuhusu kuchelewa kupatikana kwa watu wasiojulikana kwa siku 30 tangu tukio la kumpiga risasi Lissu, ambaye pia ni Mwanasheria Mkuu wa chama hicho, litokee akiwa mjini Dodoma.

Mkurugenzi wa Mafunzo na Oganaizesheni Chadema Taifa, Benson Kigaila, alisema wanapata hofu jeshi hilo linavyoshughulikia suala hilo.

Kigaila alisema jeshi la polisi linatakiwa kuwakamata wamiliki wa magari manane meupe aina ya Nissan ambayo yalikamatwa mkoani Dodoma baada ya tukio.
ads
Bonyeza HAPA kudownload applicationi ya SWAHILI NEWS kwenye simu yako ili kupata habari zetu Haraka
Share To:

SWAHIBA MEDIA STAFF

Habari , karibu katika mtandao wetu ili kuhabarika na stori zote za siku katika lugha yetu adhwim ya kiswahili, habarika wakati wote weka dunia kiganjani mwako na swahili news

Post A Comment: