MOJA ya mambo ambayo yamekuwa yakishughulisha na kufikirisha akili za watu wengi ni suala la ujenzi wa makazi. Suala hili huwa gumu kwa wenye nyumba za kupanga.


Jambo kubwa ambalo limekuwa likisababisha tafakari kubwa wakati wa mipango ya ujenzi wa nyumba ni namna ya kufanikisha gharama kubwa zinazohitajika, ambazo zinaogopesha wengi. Hizi ni kuanzia kupata uwanja, kununua vifaa na kukamilisha kazi.

Gharama ni jumla ya nguvu, rasilimali na uwezo ambao unahitajika kwa ajili ya kupata kitu ambacho kinatakiwa kwa mhusika anayehitaji kujenga makazi nyumba yake.

Katika ujenzi, gharama huangukia katika rasilimali watu na vitu hususani gharama za ufundi pamoja na nyenzo za ujenzi.

Katika mazingira ya sasa ambayo teknolojia imeendelea zaidi, ujenzi wa nyumba umekuwa ni kitu kinachohitaji utaalamu mkubwa ili uweze kukidhi sheria na miongozo iliyopo.

Miaka ya nyuma ilikuwa inawezekana kujenga nyumba kwa namna ambayo unataka mwenyewe na ingewezekana kuwa na gharama ndogo zaidi, lakini miaka ya sasa taratibu na sheria zimekuwa zikilazimu kwa namna moja ama nyingine kujenga nyumba yenye kiwango na ubora unaokubalika.

Ni muhimu kujenga nyumba ambayo imekidhi viwango vya kitaalamu na kisheria kwa manufaa bora.

Watu wengi wamekuwa wakilalamika ughali wa gharama unaotokana na kujenga kwa kufuata taratibu za kitaalamu bila kujua sababu zinazozalisha gharama hizo.

Levinus Mangula, ni mhandisi wa ujenzi, anasema zipo sababu nyingi za msingi ambazo zinafanya suala la ujenzi liwe la gharama kubwa.

Anataja sababu mojawapo kuwa ni pamoja na usanifu na mipango ya jinsi ya kufanya uamuzi wa namna jengo na mifumo yake yote inavyopaswa kuwa ikiwamo mwonekano wake, miundo, umeme, maji, mandhari na kila kitu kinacho husiana na nyumba.

Anasema hiyo ni hatua ya kwanza na ya msingi katika ujenzi na kwamba unapokosea katika hatua hiyo upo uwezekano mkubwa wa kukosea hata mwisho wa ujenzi wa nyumba husika.

“Ni muhimu kupata wataalamu ambao wamebobea katika kufanya kazi hii ya usanifu ili uweze kuweka msingi mzuri wa nyumba yako. Hatua hii huweza kuhusika pia katika kukadiria gharama ambazo nyumba yako itagharimu pamoja na muda ambao utahitajika kukamilisha ujenzi wako,” anasema Mangula.

“Lakini pia ili kupunguza gharama za ujenzi unapaswa kujenga nyumba unayoihitaji, hii inamaanisha kuwa kuna watu wanajenga nyumba ambazo hawazihitaji au hazitawasidia kwa muda ambao wamekusudia. Kujenga nyumba ambayo ni kubwa mno au ndogo sana ni sawa na kujenga nyumba ambayo huihitaji.

Hakikisha umeshirikiana na mtaalamu wako kujadiliana katika mahitaji uliyonayo na dukuduku nyingine unazozipenda ili uwe umeridhika na nyumba ambayo utaijenga.”

Mangula anashauri kutumia vizuri kila nafasi iliyopo katika eneo ulilonalo wakati wa kujenga nyumba kwa sababu ni mojawapo ya njia za kitaalam za kupunguza ghrama za ujenzi.

Anasema kila ongezeko la eneo la mita moja ya mraba katika nyumba inagharimu wastani wa Sh. 500,000 kwa nyumba ya kawaida na kwamba hiyo inatoa picha halisi ya kuepuka kuwa na nyumba inayochukua eneo kubwa bila sababu ya msingi.

“Hii inakwenda sambamba na kutumia nafasi wima (mfano kutumia makabati ya ukutani) ambayo mara nyingi imekuwa kama haitumiki lakini kama zingetumika zingepunguza mita za mraba za nyumba zisizo za lazima.

Hii inakwenda pamoja na kuepuka kuwa na korido zisizo na ulazima. Korido zinaweza kuongeza ukubwa wa nyumba mpaka asilimia 30.

Aidha anataka kuepuka kuwa na nyumba yenye konakona na umbo gumu, nyumba yako iwe na muonekano rahisi lakini mzuri,” anasema Mangula.

Jambo jingine ambalo Mangula anashauri ni kuacha kuweka vitu visivyo vya lazima katika nyumba.

“Kwa mfano unaweza kuachana na madirisha ya aluminiamu na ukatumia madirisha ya nyavu tu au ukaepuka kujenga makabati vyumbani kwani yanaweza kuongeza gharama za matofali na saruji,” anasema.

Lakini pia achana na kujenga kila kitu kwa tofali wakati mwingine kuacha nafasi kwa mfano kuwa na sebule, jiko na sehemu ya kulia isiyotengwa na kuta kunaweza pia kusaidia kupunguza gharama.

Zinapungua zaidi iwapo uezekaji utapunguza matumizi makubwa ya mbao na mabati mengi bila sababu. Ikumbukwe kutumia mbao
nyingi ni uharibifu wa mazingira hasa miti kwa vile inaondoa misitu.
ads
Bonyeza HAPA kudownload applicationi ya SWAHILI NEWS kwenye simu yako ili kupata habari zetu Haraka
Share To:

SWAHIBA MEDIA STAFF

Habari , karibu katika mtandao wetu ili kuhabarika na stori zote za siku katika lugha yetu adhwim ya kiswahili, habarika wakati wote weka dunia kiganjani mwako na swahili news

Post A Comment: