MGOMBEA uenyekiti wa CCM Wilaya ya Babati, Elizabeth Malle, amewavunja mbavu wapigakura baada ya kujinadi wakati akiomba kura kuwa ana ujauzito wa mapacha.


Katika kinyang’anyiro hicho, Elizabeth alichuana na Andrew Ombay na Peter Mchuno na kuwashinda kwa kishindo.

Hata hivyo, alisema alikuwa anamaanisha akishinda uchaguzi huo atahakikisha anarejesha Jimbo la Babati Mjini na viti vya madiwani wa kata ambavyo vilienda upinzani.

Elizabeth alishinda kwa kupata kura 149 kati ya 282. Mpinzani mwenzake Ombay alipata kura 126 na Mchuno akiambulia kura nne.

Wagombea wote walikubali matokeo, lakini Ombay alilalamika kuwapo mchezo mchafu wa  kunyimwa ushirikiano  katika kata nyingine.

Alidai kulikuwapo na dalili za rushwa huku akiwaambia wajumbe kuwa kwa sababu ni mtoto wa mkulima na mfugaji hana fedha ndio maana amenyimwa kura.

Uchaguzi huo pia uliwapata viongozi wawakilishi wa wanawake, wajumbe wa Mkutano Mkuu Taifa, wawakilishi wa vijana, wajumbe wa mkutano mkuu mkoa, wajumbe wa Halmashauri Kuu Wilaya na Katibu Mwenezi.

Mapema Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Dk. Joel Bendera, aliwaangukia wajumbe huku akiwaomba wawachague viongozi makini ili waweze kuung’oa upinzani ambao amedai unampa aibu.

Akifungua mkutano mkuu wa uchaguzi wa wilaya hiyo na jimbo kwa ujumla  watakaoongoza  chama hicho kwa miaka mitano ijayo, Dk. Bendera aliwataka wajumbe kutofanya makosa katika uchaguzi huo.

“Mimi nimechoka na ninaona aibu kubwa kukaa mahali kwenye upinzani, naomba tutangulize hekima na busara ili kumpata  kiongozi mzuri imani yako ndio ikuongoze  kumpata kiongozi anayefaa,” alisema.

Aliwataka wajumbe wa mkutano huo kuhakikisha wanawachagua viongozi makini hata kama wapo ambao waliohongwa fedha wakawape watoto wao wakale, lakini wawachague viongozi wenye kuthubutu na siyo legelege.

“Mngejua tabu ninayoipata hapa mjini mimi na Mkuu wangu wa wilaya kuwaongoza wapinzani kwa kuwa wanapanga mambo yao, kuwabadilisha ni vigumu  hivyo msituchagulie maharagwe na mbaazi  ambao watashindwa kutuvusha,” alisema.

Msimamizi wa uchaguzi  huo, Dk. Mary Nagu,  aliwataka kuona umuhimu wa kuwa na viongozi imara ili waepuke kuongozwa na upinzani katika jimbo hilo.
ads
Bonyeza HAPA kudownload applicationi ya SWAHILI NEWS kwenye simu yako ili kupata habari zetu Haraka
Share To:

SWAHIBA MEDIA STAFF

Habari , karibu katika mtandao wetu ili kuhabarika na stori zote za siku katika lugha yetu adhwim ya kiswahili, habarika wakati wote weka dunia kiganjani mwako na swahili news

Post A Comment: