ads

MWENGE wa uhuru unatarajiwa kuwasili kisiwani Unguja leo ukitokea kisiwani Pemba na kilele cha mbio hizo kitakuwa Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja.


Akizungumza na waandishi wa habari Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi, Ayoub Mohammed Mahmoud, alisema mbio hizo zitaambatana na shughuli mbalimbali ikiwamo wiki ya vijana.

Alisema mbio hizo zitazindua miradi minane ya maendeleo na miwili itakaguliwa ikiwano ya elimu, afya, umeme, viwanda na majisafi na salama.

Alisema kilele cha mbio za mwenge kitakuwa Oktoba 14, katika viwanja vya Amani Mjini Unguja na Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. John Magufuli, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika kilele hicho.

Alisema Mwenge huo utabeba ujumbe mbalimbali ikiwamo kupambana na rushwa, dawa za kulevya, Ukimwi na malaria, mambo yanayoendelea kuliangamiza taifa la Tanzania.

“Kwa kuwa kilele cha mbio za mwenge kwa mara ya kwanza kitakuwa Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja, tutakuwa na wiki ya vijana itakayoanza Oktoba 8 na kutakuwa na maandamano ambayo yanaashiria uzinduzi wa wiki ya vijana yatakayopita mbele ya mgeni rasmi Makamu wa Pili wa Rais, Balozi Seif Ali Iddi ambaye atazinduwa maonyesho hayo,” alisema.

Aidha alisema pia Oktoba 10, kutakuwa na kongamano la vijana na mada mbalimbali zitawasilishwa ikiwamo zinazohusu ujumbe wa mbio za mwenge kitaifa mwaka huu ambao ni shiriki katika kukuza viwanda kwa maendeleo ya nchi.

Alisema shughuli za viwanda zinachangia uchumi na ajira kwa nchi, hivyo vijana watapewa mwamko na uelewa kuhusiana na maendeleo endelevu ya kimataifa, watapewa uelewa kuhusu masuala ya uraia na utaifa na mchango wa vijana.

Mwenge wa Uhuru uliasisiwa mwaka 1961, ukiwa ni sehemu ya malengo ya Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, wakati akitafuta Uhuru wa Tanganyika.
ads
Bonyeza HAPA kudownload applicationi ya SWAHILI NEWS kwenye simu yako ili kupata habari zetu Haraka
Share To:

SWAHIBA MEDIA STAFF

Habari , karibu katika mtandao wetu ili kuhabarika na stori zote za siku katika lugha yetu adhwim ya kiswahili, habarika wakati wote weka dunia kiganjani mwako na swahili news

Post A Comment: