MECHI ya Ligi Kuu Tanzania Bara kati ya watani wa jadi nchini, Simba na Yanga inayotarajiwa kuchezwa Oktoba 28, mwaka huu haitafanyika kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, imeelezwa.


Akizungumza jana jijini Dar es Salaam baada ya kuutembelea Uwanja wa Taifa, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Harrison Mwakyembe, alisema uwanja huo bado unahitaji matengenezo zaidi ambayo yatachukua muda wa miezi mitatu.

Waziri Mwakyembe alisema kuwa anafahamu maombi mbalimbali yaliyowasilishwa katika wizara yake kwa ajili ya kuutumia kwenye mashindano ya kimataifa, lakini hawataruhusu kuanza matumizi mpaka pale marekebisho yake yatakapokamilika.

"Nyasi zimeota, lakini kuna sehemu kuna vipara, naomba tusiuharakishe, tuuache ukarabati wake ufanyike kwa kufuata masharti ya wataalamu, ili ubora wake uwe wa umri mrefu," alisema Waziri Mwakyembe.

Aliongeza kuwa anaamini baada ya muda huo kumalizika, Uwanja wa Taifa utakuwa ni wa kisasa na bora kuliko viwanja vingine vilivyoko katika nchi jirani zinazotuzunguka.

Alisema pia serikali itaanza mchakato wa kupata kampuni nyingine kwa ajili ya kusimamia uuzaji wa tiketi za kielektroniki baada ya mkataba uliokuwapo na Kampuni ya Selcom kumalizika.

"Itafutwe kampuni ambayo huduma zake zitakuwa zenye ubora wa hali ya juu na ambazo hazitakuwa kero kwa mashabiki, isiyokuwa na hofu, hatutaki kampuni ambayo huduma zake zinakuwa na homa wakati fulani, tunataka tufikie muda mtu ananunua tiketi anakaa nayo zaidi ya mwezi mmoja ndani kabla ya mechi haijafika," Mwakyembe alisema.

Pia aliishukuru Kampuni ya Kubashiri Matokeo ya SportPesa ambayo inazidhamini klabu za Simba na Yanga, kwa kugharamia marekebisho hayo ya uwanja ambayo yalilazimika kung'oa nyasi na kubadilisha udongo baada ya ziara ya timu ya Everton kumalizika.
ads
Bonyeza HAPA kudownload applicationi ya SWAHILI NEWS kwenye simu yako ili kupata habari zetu Haraka
Share To:

SWAHIBA MEDIA STAFF

Habari , karibu katika mtandao wetu ili kuhabarika na stori zote za siku katika lugha yetu adhwim ya kiswahili, habarika wakati wote weka dunia kiganjani mwako na swahili news

Post A Comment: