Nchi jana ilikuwa imezizima kutokana na shambulio dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu ambaye hali yake bado haijatengemaa baada ya kujeruhiwa tumboni na miguu kwa risasi.


Lissu amelazwa Hospitali ya Aga Khan jijini Nairobi alikohamishiwa juzi usiku kutoka Hospitali ya Mkoa wa Dodoma ambako alishambuliwa na watu wasiojulikana baada ya kuwasili nyumbani kwake mchana akitokea bungeni ambako alihudhuria kikao cha asubuhi.

Zaidi ya risasi 28 hadi 32 zilifyatuliwa kulenga kiti cha mbele cha upande wa kushoto wa gari aina ya Toyota Land Cruiser alichokuwa amekaa.

Tukio hilo limegusa watu wa aina tofauti tangu mtu wa kwanza alipotuma mtandaoni habari za shambulio hilo majira ya saa 8:00 mchana juzi.

Wamiliki wa akaunti za mitandao ya kijamii kama Twitter, Instagram na Facebook walichapisha picha za mbunge huyo wa Singida Mashariki na chini yake kuweka maneno ya kumuombea ili Mungu amrejeshe katika hali yake.

“Tumuombee Lissu, tuiombee nchi,” ameandika Halima Mdee, ambaye ni mbunge wa Kawe katika akaunti yake ya Twitter akiambatanisha maneno hayo na picha ya Lissu akihutubia jukwaani, akiwa amevalia magwanda ya sare za Chadema na fulana yenye michoro na rangi za bendera ya Taifa.

“Mkono wa Mungu ambao haujawahi kupungua, ukawe juu yako Mh. Lissu,” ameandika muigizaji nyota wa filamu, Elizabeth Michael, maarufu kwa kuigiza kama Lulu.

“Tumshukuru Mungu kwa afya ya Tundu Lissu hadi sasa. Kushukuru ni sehemu ya maombi#PrayForTunduLissu,” ameandika Irenei Kiria, mkurugenzi wa taasisi ya Sikika, katika akaunti yake ya Twitter.

Credit - Mwananchi
ads
Bonyeza HAPA kudownload applicationi ya SWAHILI NEWS kwenye simu yako ili kupata habari zetu Haraka
Share To:

SWAHIBA MEDIA STAFF

Habari , karibu katika mtandao wetu ili kuhabarika na stori zote za siku katika lugha yetu adhwim ya kiswahili, habarika wakati wote weka dunia kiganjani mwako na swahili news

Post A Comment: