SERIKALI ya Cuba imejenga mnara wa kumbukumbu ya mashujaa wa ukombozi wa Afrika, akiwamo baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, ikiwa sehemu ya kutambua mchango wao.


Kutokana na hatua hiyo, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, ameishukuru serikali ya Cuba kwa kutambua na kuthamini mchango mkubwa uliotolewa na mashujaa wa ukombozi wa bara la Afrika.
 
Mnara huo umejengwa katika Manispaa ya Playa, jijini Havana kwenye eneo maalum la makumbusho ya mashujaa walioshiriki katika ukombozi wa Afrika na kuwekwa   sanamu zao na maelezo mafupi ya historia zao na nchi wanazotoka.
 

Waziri Mkuu alifanya ziara katika eneo hilo juzi na kuweka shada la maua katika mnara huo uliozungukwa na sanamu za mashajuaa wa bara la Afrika na kuonyeshwa sehemu itakayowekwa sanamu ya Mwalimu Nyerere.
 
Akiwa katika eneo hilo, Waziri Mkuu aliishukuru serikali ya Cuba kwa kujenga makumbusho ya mashujaa hao na kwamba serikali ya Tanzania itashirikiana na Cuba kuhakikisha kuwa sanamu ya Mwalimu Nyerere inawekwa katika sehemu iliyotengwa.
 
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Taasisi ya Ushirikiano wa Cuba na Nchi Marafiki, Jose’ Prieto Cintado, alisema mnara huo umejengwa kwa lengo la kutambua thamani na umuhimu wa viongozi hao.
 
Mkurugenzi huyo alisema serikali ya Cuba inathamini mchango mkubwa uliotolewa na mashujaa hao katika vita ya ukombozi wa Afrika, hivyo iliamua kujenga mnara wa kumbukumbu katika nchi yao.
 
Alisema wananchi wa Cuba na watu kutoka mataifa mbalimbali ndani na nje ya Afrika, wanakwenda katika eneo hilo la makumbusho na kujifunza historia za viongozi hao. Pia eneo hilo linatumiwa na watafiti wa masuala ya kihistoria.
 
Mashujaa ambao tayari sanamu zao zimekwishawekwa kwenye eneo la kuzunguka mnara huo ni marais wa kwanza Jomo Kenyatta (Rais wa kwanza wa Kenya), Modibo Keita (Mali) na Amilcar Cabral (Guinea Bissau).
 
Wengine ni  Dk. Kwame Nkrumah (Ghana), Oliver Thambo (Kiongozi Mwandamizi wa Chama cha Ukombozi cha ANC cha Afrika Kusini), Eduardo Mondlane (Kiongozi wa ukombozi nchini Msumbuji) na Samora Machel (Rais wa kwanza wa Msumbuji).

Wengine ni Sekou Toure (Guinea), Seretse Khama (Botswana), Alhaji Aboubakar Tafawa Balewa na Obafemi Jeremiah Awolowo (Mawaziri Wakuu wa zamani wa Nigeria) na Chifu Jeremia Azikiwe (Rais wa zamani wa Nigeria).
 
ads
Bonyeza HAPA kudownload applicationi ya SWAHILI NEWS kwenye simu yako ili kupata habari zetu Haraka
Share To:

SWAHIBA MEDIA STAFF

Habari , karibu katika mtandao wetu ili kuhabarika na stori zote za siku katika lugha yetu adhwim ya kiswahili, habarika wakati wote weka dunia kiganjani mwako na swahili news

Post A Comment: