WAKATI wananchi wakilia ukata mifukoni kwa madai fedha zimetoweka kwenye mzunguko, mfanyabiashara maarufu nchini, Jaffar Sabodo (73), amemshauri Rais John Magufuli abadilishe fedha ili kubana wafanyabiashara wakwepa kodi na kuficha fedha majumbani.

Aidha, amesema kutokana na utendaji wa Rais, haoni sababu za vyama vya upinzani kuendelea kumpinga, na badala yake waache siasa na waungane naye kujenga Tanzania mpya.

Kauli ya mfanyabiashara huyo iliungwa mkono na wachumi waliozungumza na gazeti hili kubainisha kuwa njia nzuri zaidi ni Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kupunguza masharti kwa benki, hasa viwango vya riba, ili riba kwenye benki iwe kubwa jambo ambalo litafanya watu wakiweka fedha benki wapate faida.

Sabodo alitoa ushauri huo jana alipozungumza  katika mahojiano maalumu nyumbani kwake Dar es Salaam, ambapo alisema licha ya hatua nzuri za Serikali ya Rais Magufuli kiuchumi na kwenye mapambano dhidi ya rushwa, ubadhirifu na ufisadi, wapo walioficha mabilioni ya fedha nyumbani badala ya benki ili kukwepa kodi.

“Rais anafanya kazi nzuri, lakini ni wengi walioficha fedha nyumbani. Watanzania wanakufa njaa, wengine wameficha fedha. Hapo nashauri Rais abadilishe fedha hasa noti za Sh 5,000 na Sh 10,000. Hatua hiyo itasaidia kukabili ubadhirifu unaofanywa na watu wenye nia mbaya, lakini pia inaweza kuokoa uchumi na kufikia ndoto ya kuwa na Tanzania Mpya,” alisema Sabodo.

Aliongeza: “Kwa maoni yangu, hatua hiyo ya kubadilisha fedha ichukue kati ya mwezi mmoja na mmoja na nusu, watabainika wengi walioficha fedha nyumbani na hali ya uchumi itabadilika.”

Akifafanua, Sabodo ambaye ni mzaliwa wa Lindi, alisema India, Pakistan na Venezuela ziliwahi kukumbwa na hali kama iliyopo sasa nchini, lakini hatua ya kubadilisha noti ilizisaidia kuimarisha uchumi na bajeti zao.

“Watu wanaiba fedha nyingi, wanazificha chini ya magodoro, ili kumaliza hali hiyo ni muhimu noti zikabadilishwa hali itakayomlazimisha kila aliyeficha fedha kuzitoa, hapo wapo watakaokimbia nchi,” alisema Sabodo huku akitaja baadhi ya watakaokimbia hatua hiyo ikichukuliwa.

Sabodo alitoa kauli hiyo wakati Rais Magufuli ameshatoa kauli kuwataka walioficha fedha majumbani kuziacha ziingie kwenye mzunguko huku akionya wasipofanya hivyo anaweza kuamua kuzibadili ili wakose mahali pa kuzipeleka. 

Magufuli alitoa kauli hiyo Septemba kwenye mkutano wa 14 wa mwaka wa wahandisi ambapo alisema watu hao wamekuwa na utaratibu wa kutoa fedha zao benki na kuzificha kwa kuogopa kuwa atabaini kiasi walichonacho.

Wachumi
Akizungumzia suala hilo, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (Sua), Profesa Damian Gabagambi alisema: “Kuendesha uchumi hakutakiwi nguvu sana. Uchumi unajengwa kwa imani, mtu yeyote anayeendesha uchumi anatakiwa kuijenga hiyo imani na ikuzwe.

“Chochote kinachofanyika na kuua imani kinavuruga uchumi, ukiona watu wanaficha fedha hilo si tatizo, ni kwamba kuna kitu ambacho ni tatizo, kuficha fedha ndio kujihami kwao.”

Alisema njia nzuri ya kufanya watu walioficha fedha kuzitoa, ni BoT kupunguza masharti inayowekea benki, hasa viwango vya riba, ili riba kwenye benki iwe kubwa, jambo ambalo litafawanya watu kutoficha fedha kwa maelezo kuwa wakipeleka fedha kwenye benki hizo, watapata faida.

Alisema riba inayotozwa kwenye benki inapangwa na BoT na kuitaka benki hiyo kufanya marekebisho ili kusaidia wanaoweka fedha kwenye benki kupata faida.

“Ila kama wana hakika fedha zimefichwa na wahusika hawawezi kuzitoa, njia pekee ni kutishia kuchapisha, ingawa hiyo ni njia ya haraka sana. Pamoja na hayo, muhimu ni kuhakikisha chanzo cha watu kuficha fedha kinajulikana,” alisema

Mhahidhi Mwandamizi wa Chuo Kikuu Dar es Salaam (UDSM), Dk Haji Semboja alisema: “Katika uchumi ambao unakwenda vizuri na mamlaka zinazohusika na usimamizi wa fedha zinafanya kazi, suala hilo (kuficha fedha) haliwezi kujitokeza kwa maana mwenye fedha atajua jinsi ya kuziweka.

“Katika uchumi ambao watu wamekaa na kuhodhi fedha majumbani mwao ukitaka fedha hizo ziingie kwenye mzunguko basi unazibadilisha. Watu watazileta kwa nguvu maana hawatakuwa na ujanja. Ila kubadili fedha kuna sababu nyingi.”

Alisema sababu nyingine ni kutaka kubadili fedha ili kuwa na mwonekano mpya, pamoja na ubora wake ikiwa za awali zilikuwa zikichakaa mapema.

“Watu kukaa na fedha ndani ni kutoelewa mifumo ya kisasa ya kibiashara, watu wanaofanya hivyo ni wanaofanya shughuli ambazo haziko kwenye mfumo wa ulipaji kodi,” alisema.

Wapinzani

Kuhusu vyama vya upinzani, Sabodo aliyepata kufadhili Chadema na CCM, alisema kutokana na msimamo na utendaji wa Rais Magufuli vyama hivyo sasa vinaweza kuzipa kisogo siasa za majukwaani na kuungana na Rais Magufuli kujenga nchi mpya kiuchumi kwani ameonesha mwelekeo mzuri.

“Enzi za utawala wa Mkapa (Benjamin) katika utawala wa awamu ya tatu na awamu ya pili upinzani ulikuwa muhimu kuwepo, lakini sasa Rais Magufuli ameonesha nia njema na anafanya kazi kujenga Taifa akipigania wanyonge jambo lililokuwa likipigiwa kelele huko nyuma.

“Ndiyo sababu ninasema hakuna haja ya kuwa na upinzani sasa, bali wamuunge mkono Rais Magufuli tujenge Taifa,” alisema Sabodo.
DOWNLOAD APP YETU YA SWAHIBA NEWS ILI UWEZE KUPATA HABARI ZOTE MOJA KWA MOJA KUPITIA SIMU YAKO YA MKONONI BILA KUINGIA KWENYE WEBSITE,KUDOWNLOAD BONYEZA HAPA  

ANDIKA MAONI YAKO HAPO CHINI
ads
Bonyeza HAPA kudownload applicationi ya SWAHILI NEWS kwenye simu yako ili kupata habari zetu Haraka
Share To:

SWAHIBA MEDIA STAFF

Habari , karibu katika mtandao wetu ili kuhabarika na stori zote za siku katika lugha yetu adhwim ya kiswahili, habarika wakati wote weka dunia kiganjani mwako na swahili news

Post A Comment: