JESHI la Polisi limekwama kumhoji Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (Chadema), akiwa hospitalini Nairobi, Kenya.


Taarifa iliyotolewa na Lissu jana ilisema polisi wa Tanzania hawawezi kumhoji akiwa nchini Kenya au kwingineko nje ya mipaka ya nchi.

Kauli ya Lissu imekuja siku 10 tangu Mkuu wa Jeshi la Polisi, IGP Simon Sirro, kusema kuwa wametuma askari wawili kwenda Nairobi kuchukua maelezo ya Lissu, baada ya Mbunge huyo kukubali kuhojiwa.

Lissu alishambuliwa kwa risasi 32 na watu wasiojulikana mchana wa Septemba 7, mwaka huu nje ya nyumba yake Area D mjini Dodoma, wakati akitoka bungeni kwa mujibu wa Spika wa Bunge, Job Ndugai.

Kati ya risasi hizo, tano zilimpata katika sehemu mbalimbali za mwili na kusababisha alazwe hospitali tangu wakati huo na kufanyiwa operesheni 17, kwa mujibu wa Chadema.

Katika taarifa yake ya jana aliyoiweka kwenye mitandao ya kijamii, Lissu alisema polisi wameshindwa kumhoji kutokana na kasoro za kiufundi.

"Hadi sasa Mwanasheria Mkuu wa Tanzania hajamwomba Mwanasheria Mkuu mwenzake wa Kenya ruhusa ya mimi kuhojiwa na Polisi wa Kenya juu ya shambulio hilo kama inavyotakiwa na sheria husika za nchi yetu," aliandika Lissu ambaye ni mwanasheria kwa taaluma.

Alipoulizwa maoni yake juu ya kauli hiyo ya Lissu kuwa polisi hawawezi kumuhoji nje ya mipaka ya nchi, IGP Sirro aliiambia  gazeti la Nipashe “Mimi sina jibu.”

Wiki iliyopita, IGP Sirro alisema ametuma wapelelezi Nairobi baada ya kusikia Lissu amekubali kuhojiwa juu ya tukio hilo na matarajio yao pia ni kuwapata dereva na mlinzi wake.

“Tumetuma watu wetu kwenda kuchukua maelezo yake (Lissu)," alisema IGP Sirro. "Mwanzo tuliomba kwenda lakini chama (Chadema) walikataa. Juzi tumesikia wamesema wapo tayari".

"Tumetuma vijana wetu wawili kwenda Nairobi kuchukua maelezo yake.”

Alisema lengo kubwa ni kujua mazingira ya shambulio yalikuwaje na kwamba ikiwezekana wampate dereva na msaidizi huyo wa Lissu ili kurahisisha upepelezi wa tukio lenyewe.

“Upelelezi unaingia vitu vingi sana (sasa) kutompata dereva na mlinzi wake Lissu inashindwa kutupa picha kamili ya tukio,” alibainisha.

“Niwaambie Watanzania watuamini, hatuko kwa ajili ya kuona hatumtendei mtu haki, tupo kwa ajili ya kutenda haki.”
ads
Bonyeza HAPA kudownload applicationi ya SWAHILI NEWS kwenye simu yako ili kupata habari zetu Haraka
Share To:

SWAHIBA MEDIA STAFF

Habari , karibu katika mtandao wetu ili kuhabarika na stori zote za siku katika lugha yetu adhwim ya kiswahili, habarika wakati wote weka dunia kiganjani mwako na swahili news

Post A Comment: