SPIKA mstaafu wa Bunge, Pius Msekwa amesema chaguzi ndogo zinazotarajiwa kufanywa kujaza nafasi za wazi za wabunge nchini baada ya wabunge kujiuzulu au kuhama vyama vyao si matumizi mabaya ya fedha za umma, bali ndio gharama ya demokrasia ya kweli katika nchi mbalimbali duniani.
Msekwa, ambaye ni Mwanasheria na Makamu Mwenyekiti wa zamani wa chama tawala, Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania bara, amesema hayo Dar es Salaam jana, alipoulizwa maoni yake kuhusu kufanyika kwa chaguzi ndogo katika majimbo kulikotangazwa na Tume ya Taifa ya uchaguzi (NEC).
Mwanasiasa huyo mkongwe anaungana na wasomi na wanasiasa wengine nchini, waliosema katika mahojiano tofauti jana kuwa, kitendo cha wabunge, madiwani na viongozi wengine wa kisiasa kuhama vyama vyao au kujiuzulu nyadhifa walizonazo ni haki yao ya kidemokrasia na hawapaswi kulaumiwa.
Wasomi na wanasiasa hao walisema hayo walipoulizwa maoni yao kuhusu mwenendo wa siasa nchini, kutokana na wimbi la wabunge na madiwani wa vyama vya upinzani kujiuzulu nyadhifa zao na kuhamia CCM na hivyo kufanya kufanyike chaguzi ndogo.
Wamesema, kufanyika kwa chaguzi hizo ni haki ya msingi ya kikatiba kwani Tanzania imeridhia mfumo wa kidemokrasia tangu mwaka 1992 na hivyo mbunge au diwani akifa, kujiuzulu au kuvuliwa uanachama, suala la kufanyika kwa uchaguzi mdogo haliepukiki hata kama ni gharama kufanya hivyo.
Walisema hayo wakati wakizungumzia kauli ya Mbunge wa Viti Maalumu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo(CHADEMA), Upendo Peneza aliyewaambia waandishi wa habari jana kuwa, gharama za uchaguzi mdogo kwenye majimbo na kata ambako wabunge na madiwani wa vyama vya upinzani wamehamia vyama vingine ni matumizi mabaya ya kodi za wananchi, kwa kuwa ni gharama kubwa kuendesha chaguzi hizo ndogo kwa sasa.
Peneza alisema kuwa chaguzi hizo kwa ngazi ya jimbo hugharimu siyo chini ya Sh bilioni moja ambazo zingeweza kutumika katika mambo mengine. Alisema hayo akidai kukerwa na wimbi la wabunge na madiwani kujivua nyadhifa zao na uanachama wa vyama vyao na kujiunga na vyama vingine.
Alisema hatua ya wanasiasa hao inawaongezea mzigo wananchi kwa kuwa fedha zinazotumika kugharamia uchaguzi wa marudio ni kodi zao wanazolipa. Hoja hiyo ya Peneza aliyosema kuwa ni mawazo binafsi na kuwa hakutumwa na chama chake cha Chadema, imeungwa mkono na Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino cha Mwanza (SAUT), Peter Mataba aliyesema ni vyema sheria ya uchaguzi ikafanyiwa mabadiliko ili mgombea aliyefuatia wakati wa uchaguzi mkuu, apitishwe na Tume ya Uchaguzi (NEC) kuchukua nafasi husika pasipo kuingia gharama ya kufanya uchaguzi tena kila nafasi inapotokea.
Hata hivyo, Msekwa aliipinga hoja hiyo ya gharama akisema kuwa ni haki ya kidemokrasia ya wananchi kuhama vyama na uchaguzi kurudiwa. Alisema wakati Watanzania wanachagua mfumo wa kidemokrasia hawakuwa wendawazimu kwa kuwa walijua fika kwamba demokrasia ni gharama na kuongeza kuwa kupinga watu wasihame vyama na uchaguzi kurudiwa kwenye mfumo wa kidemokrasia ni udikteta ambao watu wengine wamekuwa wakiupinga pia.
“Ukimpenda mwanamke wa Kimakonde, mpende na ndonya zake. Kama tumechagua demokrasia tukubali na gharama zake. Kwa mfano huwezi kuwaambia watu kwamba tufanye uchaguzi kila baada ya miaka 10 eti kwa sababu kufanya uchaguzi kila baada ya miaka mitano ni gharama, demokrasia ni gharama, ukiikubali lazima ukubali na gharama zake,” alieleza Msekwa alipoulizwa maoni yake kuhusu kuhamahama kwa wanasiasa na madhara yake.
Post A Comment: