MKUTANO Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM)unaonza leo hapa mjini Dodoma utazaa CCM mpya kabisa kwa mara ya kwanza tangu kuwapo kwa mabadiliko ya uongozi wa mwenyekiti wa chama hicho.
Julai 23, mwaka jana, wajumbe wa mkutano huo kwa pamoja walipiga kura ya ndiyo kumuidhinisha rasmi, Rais John Magufuli kuwa mwenyekiti wa tano wa chama hicho.
Na sasa, pamoja na kupiga kura ya kuwachagua Mwenyekiti na Makamu wake wawili kutoka Zanzibar na Bara, mkutano huo pia utaanzisha awamu ya uongozi wa CCM mpya ambayo itakaa kwa kipindi cha miaka mitano inayoishia 2022, Katibu wa Nec, Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole alisema hapa jana.
Akizungumza na waandishi wa habari, Polepole aliwataja waliopitishwa kugombea nafasi hizo kuwa pamoja na Rais John Magufuli kwa nafasi ya Mwenyekiti CCM Taifa.
Polepole alikuwa akizungumza baada ya kumalizika kwa vikao vya Kamati Kuu na Halmashauri Kuu vya CCM.Wengine ni waliopitishwa kwa mujibu wa Polepole ni Makamu Mwenyekiti wa CCM Taifa Zanzibar (Ali Mohamed Shein) na Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara (Philip Mangula) ikiwa ni kipindi chake cha pili kwenye nafasi hiyo.
Alisema Kamati kuu ya CCM(CC) na Halmashauri kuu ya Taifa zilizokaa jana viliteua na kupitisha kwa kauli moja viongozi hao kugombea nafasi hizo.
“Vikao hivi vimejadili, vimetafakari na kutoa mapendekezo ya ajenda za mkutano mkuu na pia vimetoa mapendekezo ya wana CCM ambao wanaomba dhamana hizi,” alisema.
Alisema viongozi hao wanachaguliwa kwa mujibu wa Katiba ya CCM ibara ya 102 (12)(a) ambacho kinaelekeza NEC kuteua majina ya wanachama watakaogombea wa nafasi hizo.
Aidha alisema kwa kuwa chama kipo kwenye kipindi cha mpito kwa kufanya mageuzi ya kupata viongozi waaminifu, waadilifu na wachapakazi.
Alisema mkutano huo wa siku mbili unaoanza leo na kesho na utahudhuriwa na viongozi wakuu wa CCM, wastaafu na viongozi mbalimbali nchini na nje ya nchi marafiki.
Kadhalika, Polepole alisema tangu kuanza mchakato wa uchaguzi ndani ya chama hicho Aprili mwaka huu, wanachama mbalimbali zaidi ya 3,000 wamejitokeza kuwania nafasi mbalimbali ndani ya CCM.
“Kumekuwapo na mwitikio mkubwa sana wa Watanzania ambao wamependa kuwa sehemu ya historia kwa kuwamo kwenye uongozi wa CCM ambao unaishi kwenye misingi iliyoasisiwa na taifa,” alisema.
Alisema idadi hiyo ni ya wana CCM waliojitokeza kuwania kuanzia ni ngazi ya Taifa na Mikoa.
“Ngazi ya Taifa CCM tumepata mgombea mmoja nafasi ya Mwenyekiti nadhani ni tofauti na vyama vingine, na pia mgombea mmoja nafasi ya Makamu Mwenyekiti Bara, pia Zanzibar mgombea mmoja,” alisema.
Kwa upande wa mikoa, nafasi zilizogombewa ambazo tayari viongozi wake wameshapatikana ni Mwenyekiti CCM mkoa, nafasi ya ujumbe wa NEC Taifa kupitia mkoa, Katibu wa siasa na uenezi na nafasi mbalimbali zilizowaniwa kwenye jumuiya za chama hicho ambazo ni Umoja wa Wazazi, Umoja wa Wanawake(UWT) na Umoja wa Vijana(UVCCM).
Katibu huyo alisema katika nafasi ya wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (NEC) ambao watachaguliwa kwenye mkutano huo, zaidi ya wanachama 50 wamejitokeza kwenye kinyang’anyiro hicho.
Alisema wajumbe wanaotakiwa kwenye nafasi hiyo ni wajumbe 15 kutoka Zanzibar na wengine 15 kutoka Tanzania Bara.
Awali, katika kikao cha Kamati Kuu (CC), Mjumbe wa kikao hicho na Waziri Mkuu mstaafu, Salim Ahmed Salim, alitoa neno la shukrani kwa utumishi wake wa miaka mitano 2012-2017 kwa Rais Magufuli na wajumbe wake kwa uongozi mzuri, madhubuti na unaoweka mbele maslahi ya Watanzania hasa wanyonge.
Post A Comment: