Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Freeman Mbowe ameitaka serikali kubadili uamuzi wa kuzuia mikutano na shughuli nyingine za siasa kwa kuwa Tanzania ilishakubali na kuingia katika mfumo wa vyama vingi vya siasa kwa mujibu wa sheria.
Akizungumza na wananchi kwenye mkutano wake wa kumnadi mgombea wa Udiwani katika Kata ya Kitwiru Manispaa ya Iringa, Mbowe amesema serikali iliyopo madarakani imechaguliwa kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano hivyo inapaswa kuheshimu sheria pamoja na katiba hiyo ikiwemo sheria namba 5 iliyorejesha mfumo huo mwaka 1992 kabla ya hapo awali kufutwa mwaka 1965.
Kwa upande wa Mbunge wa Iringa Mjini Mchungaji Peter Msigwa amewataka wananchi wa Kata ya Kitwiru kuchagua mgombea wa Chadema ili aongeze nguvu kwenye baraza la madiwani linaloongozwa na chama hicho ambalo limeifanya Manispaa ya Iringa kuwa mfano wa kuigwa katika uendeshaji halmashauri nchini.
Naye Mgombea wa Udiwani kupitia chama hicho, Bahati Chengula amewataka wananchi kuendelea kumwamini kama walivyomwamini awali na kumchagua kuwa Mwenyekiti wa mtaa, kazi ambayo ameifanya kwa uadilifu na kujituma kwa lengo la kusukuma mbele maendeleo yao.



Post A Comment: