MCHAMBUZI wa masuala ya kisiasa nchini, Julius Mtatiro, amepongeza hatua ya Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan kumtembelea Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (Chadema), aliyelazwa jijini Nairobi, Kenya kwa ajili ya matibabu


Lissu (49), ambaye pia ni Rais wa Chama cha Wanasheria (TLS), anapatiwa matibabu ya kibingwa kwenye Hospitali ya Nairobi jijini humo tangu usiku wa Septemba 7 baada ya mchana wa siku hiyo kushambuliwa kwa kurushiwa risasi 32, kwa mujibu wa Ofisi ya Bunge, akiwa ndani ya gari lake, nyumbani kwake Area D mjini Dodoma.

Kati ya risasi hizo, tano zilimpata katika maeneo mbalimbali ya mwili wake kwa mujibu wa Chadema. 

Akimwakilisha Rais John Magufuli kwenye sherehe ya kuapishwa kwa Rais Uhuru Kenyatta jijini Nairobi juzi, Samia alitumia fursa ya kufika kwake jijini humo kumtembelea Lissu  hospitali ili kumjulia hali.

Akizungumzia suala hilo, Mtatiro alisema uamuzi huo unapaswa kupongezwa kwa kuwa Makamu wa Rais amekuwa kiongozi wa kwanza wa kiserikali kumtembelea mtaalamu huyo wa sheria hospitalini hapo.

Mtatiro alisema kuwa kutokana na uamuzi wake huo, Samia ameonyesha utu na anastahili pongezi kwa hilo.Hata hivyo, Mtatiro ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi ya Chama cha Wananchi (CUF), alisema bado kuna maswali miongoni mwa Watanzania kuhusu hatima ya kupatikana na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria waliompiga risasi Lissu.

Lissu anatarajiwa kuondolewa hospitalini hapo kabla ya mwisho wa wiki kwa ajili ya kwenda kuanza mazoezi ya viungo, ili aweze kutembea tena.

KUMSAFIRISHA NJEAkizungumza na waandishi wa habari Alhamisi iliyopita, kaka wa Tundu Lissu, wakili Alute Mughwai alisema, taratibu za kumsafirisha nje ya nchi zimeanza.

“Awamu ya tatu ya matibabu yake ni muhimu sana kwani itahusu pia mazoezi ambayo kama hayatafanyika vyema ataweza kupata ulemavu wa kudumu,” alisema Mughwai.

Mughwai alisema alizungumza na Lissu Nairobi na alimweleza kuwa akirejea nchini atakwenda katika Hospitali ya Mkoa wa Dodoma kuwashukuru madaktari na wauguzi wa Hospitali ya Mkoa kwa kuokoa maisha yake siku aliyopigwa risasi.

Wakili Mughwai alisema Lissu amemwambia baada ya hapo atakwenda kanisani na msikitini kumshukuru Mungu kwa kuokoa maisha yake kwa kufanya ibada maalumu.

“Baada ya ibada, tutaangalia utaratibu wa kifamilia kama itawezekana kwenda kufanya matambiko kwenye makaburi ya wahenga wetu 76 waliofariki katika vita miaka 200 iliyopita,” alisema.

Alisema baada ya hapo, Lissu anatarajia kuendelea kufanya kazi zake za siasa na uwakili pale alipoishia kwa ari kubwa. 
ads
Bonyeza HAPA kudownload applicationi ya SWAHILI NEWS kwenye simu yako ili kupata habari zetu Haraka
Share To:

SWAHIBA MEDIA STAFF

Habari , karibu katika mtandao wetu ili kuhabarika na stori zote za siku katika lugha yetu adhwim ya kiswahili, habarika wakati wote weka dunia kiganjani mwako na swahili news

Post A Comment: