KOCHA wa Yanga, George Lwandamina, amesema kurejea kwa mshambuliaji wake Amisi Tambwe na kiungo Papy Tshishimbi kunampa uhakika wa kuibuka na ushindi kwenye mchezo ujao dhidi ya Tanzania Prisons.


Baada ya ushindi mnono wa mabao 5-0 dhidi ya Mbeya City Jumapili iliyopita, Yanga inayodhaminiwa na Kampuni ya Kubashiri Matokeo Michezoni ya SportPesa, sasa imeelekeza nguvu zake kwenye mchezo huo ujao utakaochezwa kwenye Uwanja wa Azam Complex uliopo Chamazi nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.

Akizungumza na gazeti la  Nipashe jana, Lwandamina alisema timu yake imezidi kuimarika na ushindi dhidi ya Mbeya City unadhihirisha, hivyo kuwapo kwa nyota hao walioukosa mchezo uliopita, kunampa matumaini ya kufanya vizuri.

“Kwangu kurejea kwao kuninapa faraja na kunifanya kuwa na wigo mpaka wa kupanga kikosi, Tambwe hajacheza tangu kuanza kwa ligi na Tshishimbi hakucheza mchezo uliopita, kuwa nao wote kwa pamoja kutaongeza zaidi nguvu kuelekea kwenye mchezo dhidi ya Prisons,” alisema Lwandamina.

Tshishimbi ambaye amekuwa sehemu ya muhimili wa kikosi cha Yanga msimu huu, aliukosa mchezo uliopita kutokana na kuwa majeruhi baada ya kuumia kifundo cha mguu.

Tambwe alikuwa akisumbulia na goti, lakini amepona na Lwandamina amethibitisha kuwa anaweza akamtumia kwenye mchezo ujao.

Katika hatua nyingine, Lwandamina alisema kuwa alitegemea kupata ushindi kwenye mchezo uliopita dhidi ya Mbeya City, lakini si kwa idadi kubwa ya mabao kama waliyoyapata.

“Sikutegemea ushindi mkubwa vile, Mbeya City ni timu nzuri na inawachezaji wanaojituma, nashukuru tulitumia vizuri mapungufu yao kuweza kupata ushindi ule, ila sikutegemea kupata idadi kubwa ya mabao hasa mbele ya timu kama ile,” alisema Lwandamina.

Yanga inaendelea kushika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa Ligi Kuu ikifikisha pointi 20, mbili nyuma ya vinara Simba wanaoongoza ligi na Azam FC inayoshika nafasi ya pili ikiwa na pointi sawa na Simba, lakini ikizidiwa kwa tofauti kubwa ya mabao ya kufunga na kufungwa.
ads
Bonyeza HAPA kudownload applicationi ya SWAHILI NEWS kwenye simu yako ili kupata habari zetu Haraka
Share To:

SWAHIBA MEDIA STAFF

Habari , karibu katika mtandao wetu ili kuhabarika na stori zote za siku katika lugha yetu adhwim ya kiswahili, habarika wakati wote weka dunia kiganjani mwako na swahili news

Post A Comment: