SERIKALI imesema itakuwa tayari kuita vyombo vya kimataifa vya uchunguzi wa matukio ya kihalifu kupeleleza kushambuliwa kwa risasi kwa Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (Chadema) ikiwa vyombo vyake vya dola vitahitaji msaada wa nje.


Msimamo huo ulitolewa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa bungeni mjini hapa jana wakati akijibu swali la Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe.

Katika kipindi cha 'Maswali kwa Waziri Mkuu', Mbowe ambaye pia ni Mbunge wa Hai alitaka kujua sababu za kile alichokiita kigugumizi kwa serikali kuita wataalamu wa kimataifa kuchunguza tukio la kushambuliwa kwa mwanasheria huyo wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).

Miongoni mwa mashirika maarufu ya upelelezi duniani, na ambayo baadhi ya watu wamekuwa wakiyataja kila inapoibuka hoja ya kuhitaji msaada kutoka nje ni pamoja na Central Intelligence Agency (CIA) la Marekani na Scotland Yard la Uingereza.

Awali, akijenga hoja yake, Mbowe alisema katika siku za karibuni kumekuwapo matukio mengi yanayovunja usalama, amani na kujenga chuki miongoni mwa vyama vya siasa na kuharibu utengamano wa kitaifa.

Alisema tukio la kushambuliwa risasi kwa Lissu limezua hofu kubwa si tu kwa taifa, bali katika Bara la Afrika na jumuiya ya kimataifa, hivyo kuharibu sura ya taifa na heshima yake.

"Na hatujaona kama serikali imechukua hatua yoyote ili jambo hili lisiendelee kuharibu sura ya taifa," Mbowe alisema na kufafanua zaidi:

"Pia kulitokea vifo vya kisiasa. Alifariki mwenyekiti wetu wa Geita, serikali ikasema inafanya uchunguzi, mpaka leo hakuna. Msaidizi wangu Ben Saanane, nikakuomba Waziri Mkuu serikali yako uiruhusu uchunguzi wa kimataifa ili kutatua tatizo hili, ukasema vyombo vya ndani vina uwezo, hadi leo hakuna kitu.

"Pia tumeomba kushambuliwa kwa Lissu kuchunguzwa na vyombo vya kimataifa vya uchunguzi vilivyo huru, bado serikali inaonekana ina kigugumizi katika jambo hili.

Unatupa kauli gani sisi kama chama, wabunge na taifa?"

Katika majibu yake, Waziri Mkuu Majaliwa, alisema amani na utulivu ndani ya nchi ni jambo ambalo lazima Watanzania washikamane na washirikiane katika kulidumisha kwa kuwa ndilo linaendelea kuipa nchi heshima duniani.

Alisema vyombo vya dola vinaendelea kuchunguza tukio la kushambuliwa kwa mbunge huyo (Lissu) na matukio mengine ya kihalifu yaliyotokea nchini.

"Yapo matukio yanajitokeza, Mbowe umezungumzia upande wa kisiasa, lakini matukio haya yapo kwa ujumla wake nchini kwenye maeneo kadhaa na maeneo ya mikusanyiko, na watu wengine …wako wenzetu ambao hawana nia njema wanatenda matukio hayo," alisema Majaliwa.

Kiongozi huyo wa serikali aliongeza: "Na hata hili la Lissu, hatukupenda mambo kama hayo yatokee, lakini pia tumepoteza Watanzania wengi. Nakumbuka Wilaya za Mkuranga, Kibiti na Rufiji, hata kamanda wa jeshi la ulinzi nchini alipigwa risasi.

"Kwa hiyo, tuzungumze kwa ujumla wake na kwa utamaduni ambao tumeujenga katika nchi hii katika kujilinda wenyewe na kuhakikisha nchi inakuwa salama. Nikuhakikishie kwamba vyombo vya dola vinaendelea kufanya uchunguzi wa haya.

"Na uchunguzi huu hauwezi kuwa wa leo leo ukapata ufumbuzi kwa sababu wanaotenda matendo haya wanatumia mbinu nyingi za kujificha. Kwa hiyo na sisi lazima tutumie mbinu zetu za kutambua hao waliotenda hayo katika kila eneo ili tuweze kutoa taarifa ya jumla.

"Nikuhakikishie kwamba vyombo vya dola havipo kimya,  vinaendelea…pia vina uwezo wa kusimamia usalama ndani ya nchi. Ni suala la muda na taratibu gani zichukuliwe. Hilo linategemea na waliotenda matukio na namna ambavyo wamejificha na namna ambavyo na sisi tunatumia njia mbalimbali za kuweza kuyapata haya na kutoa taarifa kwa Watanzania.

"Nikusihi na familia zote ambazo zimepata athari na zimeripoti polisi, vyombo vya dola… kwamba pale ambapo tutakamilisha uchunguzi tutatoa taarifa kwa familia, ndugu au jamaa na kuwaambia hatua ambazo tumechukua."

Aidha, Majaliwa aliwataka wananchi kuendelee kujenga imani kwa vyombo vya dola akisisitiza kuwa vikikamilisha uchunguzi wa matukio hayo vitatoa taarifa kwa umma.
Hata hivyo, baada ya majibu hayo ya Waziri Mkuu, Mbowe alisimama na kueleza kuwa tukio la kushambuliwa kwa Lissu linapaswa kupewa uzito wa juu.  

"Nakubaliana na maisha ya kila Mtanzania yana thamani, ila swali langu lilikuwa specific (mahsusi) ya jambo linaloitwa political persecution, tukio la kushambuliwa Lissu si la kawaida na tusilichanganye na matukio mengine," Mbowe alisema. "Uonevu dhidi ya viongozi na wanachama wa upinzani umekuwa utamaduni wa kawaida. 

"Vyombo vya dola vinatesa watu, vinaumiza watu, leo (jana) ni siku ya tatu, (tangu) mbunge wangu wa Ndanda, Cecil Mwambe amekamatwa na polisi Mtwara na yupo mahabusu zaidi ya saa 48. Kisa alikuwa anafanya mkutano wa kampeni ya uchaguzi katika kata mojawapo pale Mtwara mjini.  

"Polisi wakamshika, huyu ni mbunge na mwenyekiti wa kanda ya kusini yupo ndani siku ya tatu sasa, uonevu unaendelea na katika uchaguzi huu wa marudio viongozi wetu wanakamatwa, wanateswa," aliongeza Mbowe.

Pia Mbowe alisema haitakuwa mara ya kwanza kwa serikali kuita vyombo vya kimataifa vya uchunguzi kwa kuwa ilishawahi kuviita vyombo vya uchunguzi vya nje, akitolea mfano wakati Benki Kuu (BoT) ilipoungua Scotland Yard waliitwa kufanya uchunguzi nchini na hilo ni jambo la kawaida katika jamii ya kimataifa.

"Ni kwa sababu vyombo vya dola tumevi-suspect (tumevituhumu) havikuchukua tahadhari kulinda viongozi, havikuchukua hatua za mapema kuzuia uhalifu ule, aidha kwa kutaka au kwa kushiriki," Mbowe alisema.

Aliongeza kuwa ana imani na vyombo vya ndani kuwa na uwezo na havidharau, lakini akadai hakuna dhamira ya kuchunguza tukio hilo.

"Na kwa sababu hakuna dhamira, serikali itoe clearance waje watu wafanye uchnguzi ili jambo hili likomeshwe. Kwanini sasa usikubali kwa niaba ya serikali uruhusu vyombo vya kimataifa ili tukate mzizi wa fitina?" Mbowe alihoji.

Akijibu swali hilo, Waziri Mkuu Majaliwa alisema vyombo vya dola ndiyo vina nafasi nzuri zaidi ya kusema kama vinahitaji msaada wa vyombo vya nje kuchunguza tukio hilo.

Alisema serikali imesikitishwa na tukio la kushambuliwa kwa mbunge huyo na mauaji yaliyofanyika nchini hivi karibuni na inaviamini vyombo vyake katika kuwasaka wahusika.

"Inabidi vyombo vya usalama vikamilishe kazi yao ndipo vije viseme," Waziri Mkuu alisema na kuongeza:

"Hakuna mtu yeyote aliyefurahishwa na tukio la Lissu au ya mauaji au mashambulio au migongano inayoendelea kwenye jamii yetu. Lakini vyombo vya dola tumevipa jukumu la kusimamia, la kulinda usalama wa raia na mali zao kwa kiwango kinachotakiwa.

"Na pale ambapo kuna tatizo, vyombo vya dola vina jukumu la kukamata wale wote waliohusika, ila wanaotenda makosa ni watu ambao wanakuwa wamejiandaa pia kuficha uovu wao dhidi ya vyombo vya dola. Si kwamba vyombo vya dola havina uwezo wa kufanya kazi yake.

"Matukio yote yametokea katika kipindi kifupi. Kusema masuala ya Kibiti na Mkuranga si kwamba naficha tukio hilo la Lissu lisitambulike. Tunachukua mwenendo wa tukio na uwezo wa vyombo vyetu kuhakikisha tunabaini matukio.

"Ndiyo maana nasisitiza kwa Watanzania kuwa lazima tushirikiane katika kulinda nchi yetu na kila mmoja atoe taarifa na mwenye ushahidi katika jambo ili vyombo vya dola viweze kufanya kazi kwa urahisi.

"Najua unazungumzia Lissu anatoka upande wako. Lakini Lissu ni mbunge mwenzetu, ni letu pia, lazima tushirikiane. Hivyo nikuhakikishie jambo hili linapata mwelekeo.

"Kwa hiyo nikuhakikishie vyombo vyetu uwezo upo, lakini pale ambapo wataona kuna umuhimu huo vyombo vyenyewe  vinaweza vikalieleza … lakini mimi siwezi kulihakikishia taifa kuwa tumekosa uwezo kwa sababu tunaamini vyombo vyetu vina uwezo wa kufanya uchunguzi.

Waziri Mkuu alisema Mbowe anapaswa kuamini serikali inayo nia njema na familia ya wale wote walioathirika, na inayo nia njema ya kukamata na pia kulinda amani ya nchi ili kila mmoja awe na uhakika wa shughuli anazofanya kila siku.

Alisema serikali itaendelea kufanya kazi hiyo na kuwasiliana na kiongozi huyo wa upinzani ili kuona namna ya kutatua matatizo yanayojitokeza kwenye maeneo mbalimbali nchini.

Lissu (49), ambaye pia ni Rais wa Chama cha Wanasheria (TLS) na Mwansheria wa Chadema, alishambuliwa kwa kupigwa risasi zaidi ya 20 na watu wasiojulikana akiwa ndani ya gari lake alipofika nyumbani kwake mjini Dodoma akitokea bungeni mchana wa Alhamisi ya Septemba 7, mwaka huu.

Baada ya tukio hilo, alikimbiziwa katika Hospitali ya Rufani ya Mkoa wa Dodoma kabla na baadaye kupelekwa kwa ndege jijini Nairobi, Kenya kwa matibabu zaidi. Hadi sasa, hakuna taarifa yoyote rasmi ya polisi juu ya kukamatwa kwa yeyote kuhusiana na tukio hilo.  
ads
Bonyeza HAPA kudownload applicationi ya SWAHILI NEWS kwenye simu yako ili kupata habari zetu Haraka
Share To:

SWAHIBA MEDIA STAFF

Habari , karibu katika mtandao wetu ili kuhabarika na stori zote za siku katika lugha yetu adhwim ya kiswahili, habarika wakati wote weka dunia kiganjani mwako na swahili news

Post A Comment: