KOCHA wa Yanga, George Lwandamina, ameonyesha kiu ya kupunguza wigo wa mabao kutoka kwa watani zao Simba, baada jana kuwahenyesha washambuliaji wa timu hiyo kwenye mazoezi ya asubuhi akiwapa mbinu maalum za kutupia.


Yanga inayodhaminiwa na Kampuni ya Kubashiri Matokeo Michezoni ya SportPesa kama ilivyo kwa Singida United na watani zao, Simba, ina pointi 16 sawa na Mtibwa Sugar na Azam FC, lakini Wekundu wa Msimbazi hao wapo kileleni mwa msimamo wa ligi kutokana na tofauti kubwa ya mabao ya kufunga na kufungwa.

Simba imeshatupia mabao 20 na kuruhusu matano wakati Yanga ikiziona nyavu mara 11 na nyavu zao zikitingishwa mara nne wakati huu timu zote zikiwa zimeshuka dimbani mara nane.

Yanga jana ilianza mazoezi ya uwanjani baada ya juzi kujifua gym ikijiandaa na mchezo wao dhidi ya Singida United utakaochezwa Jumamosi ijayo mkoani Singida.

Katika mazoezi hayo ya jana asubuhi, washambuliaji wakiongozwa na Ibrahim Ajibu na mawinga walifanya mazoezi maalum ya kufunga kwa kupokea mipira kutoka kwa viungo na kuitumia kufunga huku pia wakifanyia kazi kucheza mipira ya krosi.

Lwandamina, aliliambia gazeti la Nipashe kuwa zipo kasoro alizoziona kwenye mchezo wao uliopita dhidi ya Simba na ameamua kuzifanyia kazi mapema kabla ya mchezo wao ujao.

“Mchezo uliopita pamoja na ugumu wake, bado tulifanikiwa kutengeneza nafasi, lakini hatukuzitumia, kama tungekuwa makini basi matokeo yangekuwa tofauti na tuliyoyapata,” alisema Lwandamina.

“Lazima tutumie vyema nafasi tunazozipata, tutaendelea kuzifanyia kazi kwenye mazoezi yetu,” aliongeza kusema.

Aidha, Kocha huyo alisema mchezo wao ujao dhidi ya Singida United hautakuwa rahisi na wanajiandaa kukabiliana na moja ya timu ngumu kwenye ligi.

“Si timu ya kubeza, wamepata matokeo mazuri kwenye michezo yao iliyopita na pia nimeambiwa wamesajili vizuri hivyo lazima tuwe makini nao,” alisema Lwandamina akiuzungumzia mchezo ujao.

Wakati huo huo, Meneja wa Yanga, Hafidh Saleh, aliliambia Nipashe kuwa safari yao ya kuelekea Singida wameisogeza mbele na sasa wataondoka Dar es Salaam kesho.

Awali kikosi cha timu hiyo kilipanga kuondoka leo kuelekea Singida, lakini uongozi pamoja na benchi la ufundi wamekubaliana timu iondoke kesho.

Mchezo huo wa tisa kwa timu hizo msimu huu, utachezwa kwenye Uwanja wa Namfua mjini Singida baada ya wenyeji kurejea kwenye uwanja wao huo wakitokea Dodoma walikokuwa wakiutumia Uwanja wa Jamhuri kupisha marekebisho kwenye Namfua.
ads
Bonyeza HAPA kudownload applicationi ya SWAHILI NEWS kwenye simu yako ili kupata habari zetu Haraka
Share To:

SWAHIBA MEDIA STAFF

Habari , karibu katika mtandao wetu ili kuhabarika na stori zote za siku katika lugha yetu adhwim ya kiswahili, habarika wakati wote weka dunia kiganjani mwako na swahili news

Post A Comment: