Wakati jana Jumapili dunia imeadhimisha siku ya wazee, Baraza la Wazee wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) limemwomba Rais John Magufuli kukutana na wazee nchini ili kujadiliana na kupata ufumbuzi wa masuala mbalimbali.


Wito huo umetolewa jana na katibu mkuu wa baraza hilo, Roderick Lutembeka wakati akizungumza na waandishi wa habari makao mkuu wa Chadema jijini Dar es Salaam kuhusu siku ya wazee duniani.

"Wazee ambao tunashauri Rais Magufuli akutane nao ni wazee kutoka vyama vya siasa, viongozi wastaafu wa dini, wastaafu serikalini na awe tayari kupokea ukosoaji wao na kuufanyia kazi," amesema Lutembeka.

Amesema mchakato wa Katiba uliokwama unapaswa kupatiwa ufumbuzi ili kuleta tija kwa Taifa kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.

"Umuhimu wa Taifa kuwa na Katiba mpya unazidi kuonekana kila siku...Watanzania wanataka Katiba mpya kwa ajili ya kutibu majeraha ya Taifa hili," amesema.

 Kuhusu wazee, Lutembeka amesema wamekuwa hawathaminiwi na kutambulika katika ngazi za uamuzi, afya na ndani ya jamii.

Amesema ni wakati sasa kwa Serikali kupeleka muswada wa sheria ya wazee bungeni ili kutekeleza Sera ya Taifa ya Wazee ya Mwaka 2003.

Lutembeka amesema kama Serikali haitafanya hivyo, wawakilishi wa wananchi ambao ni wabunge watumie kanuni ya Bunge kuwasilisha muswada binafsi kuhusu sheria ya wazee nchini.


ads
Bonyeza HAPA kudownload applicationi ya SWAHILI NEWS kwenye simu yako ili kupata habari zetu Haraka
Share To:

SWAHIBA MEDIA STAFF

Habari , karibu katika mtandao wetu ili kuhabarika na stori zote za siku katika lugha yetu adhwim ya kiswahili, habarika wakati wote weka dunia kiganjani mwako na swahili news

Post A Comment: