Rais John Magufuli ametangaza kiama kwa benki zinazofanya vibaya nchini pamoja na kampuni ambazo hazijajiunga katika mfumo data na ukusanyaji mapato kwa njia ya kieletroniki baada ya kuagiza kuwa zifungiwe kufanya kazi.


Akizungumza katika uzinduzi wa tawi la Benki ya CRDB la LAPF mjini hapa, Rais Magufuli alisema Juni mwaka huu alizindua mfumo wa data na ukusanyaji mapato kwa njia ya kieletroniki na aliagiza benki kujiunga na mfumo huo.

Alisema kamishna wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) aliahidi kuwa hadi kufikia mwezi huu kampuni zote za benki na simu zitakuwa zimejiunga.

Alisema hadi kufikia katikati ya Desemba, anazo taarifa kuwa ni benki chache na kampuni ambazo zimejiunga na mfumo huo.

“Napenda kurudia, benki na kampuni za simu zinazotaka kufanya biashara nchini zihakikishe zinajiunga na mfumo huo kabla ya mwaka huu kuisha. Kwa kampuni ya simu itakayoshindwa kutekeleza agizo hili taratibu husika zifanyike ikiwezekana kampuni au benki zifungiwe kufanya kazi nchini,” alisema. Aliitaka Benki Kuu Tanzania (BoT) kusimamia vizuri benki zinazoanzishwa nchini akitoa mfano kuwa iliwahi kufungua benki ambayo makao makuu yake yako Tanzania lakini fedha zilizokuwa zimewekwa nchini ni chini ya asilimia 10 na kiasi kilichobakia kiliwekwa katika nchi ambayo ina mambo ya ajabuajabu.

“Na mlifungua, mlikuwepo na kuna PhD zaidi ya 17 pale lakini mkaruhusu mambo ya kipumbavu na kishenzi kufanyika mpaka ile benki ilipofungiwa Marekani na wao ndio wakatambua kwamba hii ni ya ajabu vitu hivi vinatia aibu,” alisema.

Aliiagiza BoT kutosita kufuta benki ambazo hazifanyi vizuri nchini hata kama ni ya Serikali na kwamba biashara haina siasa.

“Nataka katika wakati wangu tuache haya mambo tuliyoyazoea ya kubebanabebana. Benki inataka kufilisika mnaomba fedha kutoka Hazina na zinapelekwa kule kwenda kusaidia. Hiyo hapana, nataka fedha tulizo nazo ziende kuhudumia wananchi kwa kutoa huduma.

“Asiyeweza kushinda afe potelea mbali bora tubaki hata na benki tano ambazo zinafanya kazi vizuri kuliko kuwa na mabenki ya kuwabebabeba for political reasons (kwa sababu za kisiasa),” alisema.

Pia, Rais Magufuli alitaka BoT na Wizara ya Fedha kuangalia suala la matumizi ya dola akisema haiwezekani nchi ikawa na matumizi ya aina mbili au tatu ya fedha.

Alisema kuruhusu hilo kutaharibu uchumi wa nchi na kuionya BoT kuepuka kuwa sehemu ya kuua uchumi wa nchi.

“Mbaya zaidi haya yamekuwa yakifanywa na BoT, mnapotangaza tender (zabuni) zenu hata wafagiaji mnawalipa kwa dola. Nilizuia contract (mkataba) moja ambayo nyinyi mlikuwa mmeipanga. Haiwezekani nyie wasimamiaji wa fedha nyinyi haohao mnakuwa watumiaji wabaya wa ku-control (dhibiti) fedha za nchi,” alisema.

Aliitaka BoT kuchukua hatua katika vituo vya kubadilishia fedha na kwamba wakati akizungumza, zaidi ya dola bilioni moja za Marekani zimekamatwa uwanja wa ndege.

“Zilikuwa zinaingizwa Tanzania na hujui zilikuwa zinaenda wapi. Ni kwa sababu Tanzania kumeshaonekana ni kichaka cha fedha za kigeni na inawezekana ikawa hata money laundering (utakatishaji fedha) ikawa inafanyika,” alisema.

Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB, Dk Charles Kimei alisema benki hiyo yenye matawi 260 nchini pamoja na huduma nyingine zikiwamo Saccos, inawahudumia wateja milioni 3.5 nchini.

“Kuanzia 2005 CRDB imekuwa ni benki inayoongoza hapa nchini kwa ukubwa wa amana ambazo zimefikia Sh4.1 trilioni, rasilimali Sh5.5 trilioni ni pesa nyingi sana. Tuna mikopo tuliyotoa na inaendelea kuzunguka Sh3.5 trilioni. Hakuna mfanyabiashara ambaye maisha yake katika shughuli za biashara au nyingine hajaonja mkopo wetu,” alisema.
ads
Bonyeza HAPA kudownload applicationi ya SWAHILI NEWS kwenye simu yako ili kupata habari zetu Haraka
Share To:

SWAHIBA MEDIA STAFF

Habari , karibu katika mtandao wetu ili kuhabarika na stori zote za siku katika lugha yetu adhwim ya kiswahili, habarika wakati wote weka dunia kiganjani mwako na swahili news

Post A Comment: