WAKILI wa utetezi katika kesi ya uhujumu uchumi na kutakatisha fedha inayomkabili mfanyabiashara Harbinder  Sethi na mwenzake, Alex Balomi, amedai mahakamani kuwa puto lililomo tumboni mwa Seth limeisha muda wake na asipobadilishwa linaweza kumsababishia kifo.


Kadhalika amedai kuwa wanawasilisha hoja hiyo kwa sababu mshtakiwa alipelekwa kufanyiwa matibabu Hospitali ya Taifa Muhimbili lakini hadi leo (jana) hajapatiwa majibu.

Balomi alitoa madai hayo jana mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam.

Mbali na Sethi mshtakiwa mwingine ni James Rugemarila na wote kwa pamoja wanakabiliwa na mashtaka  12 ya  uhujumu uchumi, kutakatisha fedha  na kuisababishia serikali hasara ya Dola za Marekani 22,198,544.60 na Sh. 309,461,300,158.27.

Awali, upande wa Jamhuri ukiongozwa na Wakili wa Serikali Leornad Swai, ulidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika, hivyo kuomba tarehe nyingine ya kutajwa.

"Mheshimiwa Hakimu mshtakiwa Sethi ana puto tumboni. Tangu awekewe  limeisha muda wake, hivyo linapaswa kubadilishwa mwishoni mwa mwezi Oktoba," alidai na kuongeza:

"Kama puto hilo halitabadilishwa kama alivyopangiwa linaweza kugeuka sumu na kuondoa maisha yake.  Tunaomba daktari aliyechukua vipimo anapaswa kumpatia majibu ili mshtakiwa ajue hatima yake," alidai Balomi.

Aidha, alidai kuwa upande wa utetezi wanaomba upelelezi ukamilike kwa sababu upande wa Jamhuri unaonekana umezembea na watuhumiwa wanateseka mahabusu bila sababu.

Swai alidai kuwa Sethi alipelekwa hospitalini Oktoba 13, mwaka huu, na kupata matibabu kutokana na vipimo vya daktari, lakini majibu ni siri ya daktari na mshtakiwa na si suala la  kuzungumzia mahakamani, upelelezi tunaendelea kufanyia kazi.

Hakimu Shaidi alisema mahakama yake ilitoa amri kwamba Sethi apelekwe hospitalini na amepelekwa kwa hiyo daktari amekamilisha kazi yake, mawakili wanaweza kwenda kuulizia kuhusu vipimo vyake.

Pia alisema upande wa mashtaka ufanye unavyoweza kuhakikisha upelelezi unakamilika. Kesi hiyo itatajwa Novemba 10, mwaka huu.
ads
Bonyeza HAPA kudownload applicationi ya SWAHILI NEWS kwenye simu yako ili kupata habari zetu Haraka
Share To:

SWAHIBA MEDIA STAFF

Habari , karibu katika mtandao wetu ili kuhabarika na stori zote za siku katika lugha yetu adhwim ya kiswahili, habarika wakati wote weka dunia kiganjani mwako na swahili news

Post A Comment: