SERIKALI imeunda timu maalumu ya wataalamu 11 kwa ajili ya kuchunguza ubora wa vichwa 13 vya treni vilivyotelekezwa katika bandari ya Dar es Salaam.


Wakati timu hiyo ikiundwa, serikali imesema itavinunua vichwa hivyo endapo vitabainika kuwa katika ubora.

“Tukishajiridhisha kwenye ubora wa vichwa vile tutakaa na walioleta vichwa na kuanza kuzungumza kwani nia ya serikali ni kufanyakazi na wadau mbalimbali.

Tukishajiridhisha kama vichwa vile vipo katika ubora unaotakiwa  baadaye tuweze kuvinunua na kuanza kutumika,” alisema jana Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarwa, alipofanya ziara bandarini kukagua ujenzi wa mashine za ukaguzi (scanner).

“Kama mnavyojua tunajenga miundombinu mingi hapa kwenye bandari yetu na bila kuwa na treni iliyo imara na vichwa vilivyo imara na vya kutosha hatutaweza kuhudumia mizigo yote inayopita katika bandari yetu ya Dar es Salaam.”

Alisema kwa kutambua jambo hilo, serikali imeona kuna haja ya kufanya tathimini ya vichwa hivyo  na kwamba kuna wataalamu wazuri wa kukagua ili kupata ubora wake.

Alisema timu hiyo itamaliza kazi yake ndani ya siku 10 zijazo na kwamba tangu waanze tathimini hiyo wana siku nne.

Julai, mwaka huu, Rais John Magufuli alipofika bandarini hapo kwa ajili ya uwekaji wa jiwe la msingi upanuzi wa bandari ya Dar es Salaam, aliagiza apatiwe maelezo kuhusiana na vichwa hivyo pamoja na mmiliki wake.

Rais Magufuli alisema kuwa ana taarifa ya uwepo wa vichwa 13 vya treni bandarini hapo ambavyo mmiliki wake hajulikani na kwamba inaelezwa kuwa ni vibovu.

Hata hivyo, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Deusdedit Kakoko, alisema vichwa hivyo vina nembo ya TRL (Kampuni ya Reli Tanzania) na kwamba ulitokea mgogoro kati ya TRL na kampuni iliyotengeneza baada ya kubainika kuwa mchakato mzima wa manunuzi haukuwa sahihi.

TRL ilinunua vichwa 15 vya treni kutoka kampuni ya EMD (Electro-Motive Diesel)ya Marekani na utengenezaji wake ukafanywa na Kampuni ya DCD ya Afrika Kusini.

Kuhusu ujenzi wa mashine za scanner, Profesa Mbarawa alisema unatarajia kukamilika mwezi ujao na kwamba utaimarisha ulinzi zaidi bandarini na kusimamia mapato kikamilifu.

Ujenzi wa mashine hizo mbili ambazo umegharimu Sh. bilioni 27 na kwamba mashine hizo ni muhimu  kwa usalama wa bandari  na zitasaidia kuimarisha ulinzi. pia alisema ni za kisasa na zina uwezo mkubwa wa kutambua vitu vya aina mbalimbali ambavyo vitapita bandarini hapo.
ads
Bonyeza HAPA kudownload applicationi ya SWAHILI NEWS kwenye simu yako ili kupata habari zetu Haraka
Share To:

SWAHIBA MEDIA STAFF

Habari , karibu katika mtandao wetu ili kuhabarika na stori zote za siku katika lugha yetu adhwim ya kiswahili, habarika wakati wote weka dunia kiganjani mwako na swahili news

Post A Comment: