Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe amesema milango iko wazi kwa aliyekuwa mbunge wa Singida Kaskazini (CCM), Lazaro Nyalandu kujiunga na chama hicho na kuwakaribisha wengine wanaochukizwa na yanayoendelea CCM.


Akizungumza jana muda mfupi baada ya Nyalandu kutangaza kujiondoa CCM, Mbowe amesema, “Chadema si ya Mbowe ni ya Watanzania, tunamkaribisha sana aje tuendeleze mapambano kwani Chadema si ya mtu.”

Mbowe ambaye pia ni Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani bungeni amesema hoja alizozitoa Nyalandu ndiyo kilio chao cha muda mrefu na kitendo chake cha kusimama hadharani na kueleza yote ni ujasiri na wengine wanapaswa kuiga mfano wake.

“Tunawakaribisha na wengine wanaochukizwa na yanayoendelea, wapo mawaziri, wabunge, Ma-RC (wakuu wa mikoa), Ma-DC (wakuu wa wilaya) na viongozi wengine wanachukizwa na ukandamizaji unaofanywa, tunawakaribisha sana, wasiogope kusema ukweli na kusimamia yale wanayoamini,” alisema

Mbowe alisema, “tunamkaribisha hata kama kuna makosa aliyoyafanya huko nyuma kama tulivyo na makosa sisi wengine, tunamkaribisha aje tufanye mambo mema kwani tunaambiwa hakuna urafiki wa kudumu au uadui wa kudumu.”

Lowassa: Tumelamba dume

Kwa upande wake Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Edward Lowassa amemkaribisha Nyalandu.

Akionyesha kuwa na furaha alipozungumza na gazeti la  Mwananchi jana Lowassa hakuwa na maneno mengi, akiyafupisha kwa kusema “tumelamba dume”.

Nyalandu (47), ambaye pia alikuwa mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM, alitumia nafasi hiyo kuomba kujiunga na Chadema, akisema anaiomba imfungulie mlango.

“Mbona amechelewa?Alitakiwa awe amejiunga muda mrefu, tena hasa wakati wa Uchaguzi Mkuu. Ninamkaribisha sana kwa sababu ni mwanasiasa mzuri na anayejua majukumu yake,” alisema Lowassa ambaye alikuwa waziri mkuu wa kwanza katika Serikali ya Awamu ya Nne.

“Nyalandu ni hazina, ni mbunge imara na ni mwanasiasa wa mfano,” alisema Lowassa, ambaye alijiunga na Chadema mwaka 2015 na kuwania urais kupitia muungano wa Umoja wa Katiba ya Watanzania (Ukawa).

Lowassa alimsifu Nyalandu kwa kuisaidia jamii na akatoa mfano jinsi alivyosaidia watoto watatu wa Shule ya Lucky Vincent waliokwenda kutibiwa Marekani baada ya kupata ajali ya basi iliyoua wanafunzi 32, walimu wawili na dereva mmoja.

“Nyalandu ana contacts (anafahamu watu wengi) nyingi na jumuiya ya kimataifa ni bidhaa nzuri kuwa nayo,” alisema Lowassa, ambaye katika uchaguzi wa urais alishika nafasi ya pili kwa kupata kura 6,072,848 (asilimia 39.97) ikiwa ni rekodi ya kura nyingi kwa upinzani tangu mfumo wa vyama vingi urejeshwe mwaka 1992.

Zitto amwambia ni uamuzi sahihi

Mbunge wa Kigoma Mjini(ACT Wazalendo), Zitto Kabwe amempongeza Nyalandu kupitia ujumbe wake aliouandika Facebook akisema ameonyesha uongozi.

“Lazaro Nyalandu, uomeonyesha uongozi. Kwa namna haki za watu zinavyovunjwa na uchumi wa nchi unavyoporomoka, unahitaji roho ngumu sana kuwa CCM. Umefanya uamuzi sahihi, wakati sahihi kwa sababu sahihi. Kila la heri,” alisema Zitto.

Mbunge wa Bukoba Vijijini ambaye pia ni Mwenyekiti wa Wabunge wa CCM, Jason Rweikiza alipoulizwa kwa njia ya simu alicheka kisha akasema hawezi kuzungumza kwa wakati huo.

Viongozi wengine wa CCM akiwemo Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole hawakupokea simu wala kujibu ujumbe kila walipotafutwa.
ads
Bonyeza HAPA kudownload applicationi ya SWAHILI NEWS kwenye simu yako ili kupata habari zetu Haraka
Share To:

SWAHIBA MEDIA STAFF

Habari , karibu katika mtandao wetu ili kuhabarika na stori zote za siku katika lugha yetu adhwim ya kiswahili, habarika wakati wote weka dunia kiganjani mwako na swahili news

Post A Comment: