IKIWA imebakia siku moja kabla ya mchezo wa watani wa jadi, Kocha wa Yanga, George Lwandamina, amesema kwake ni pigo kuwakosa nyota wake wa kimataifa, Amis Tambwe, Donald Ngoma na Thaban Kamusoko kwenye mchezo huo wa kesho.


Yanga ambayo inarejea leo jijini Dar es Salaam ikitokea Morogoro ilipoweka kambi kujiandaa na mchezo wa kesho dhidi ya Simba, itakosa huduma ya wachezaji hao ambao walibaki Dar es salaam kujiuguza majeraha yao.

Akizungumza na gazeti la Nipashe, Lwandamina, alisema kuwa kukosa huduma ya nyota hao kwenye mchezo mkubwa na wenye upinzani kama wa kesho ni changamoto kwake.

“Nashukuru wachezaji wangu wapo katika ari nzuri, lakini kama mnavyojua Tambwe, Ngoma na Kamusoko hatupo nao huku (Morogoro) wapo Dar es Salaam wakiendelea kujiuguza, nilitamani sana kuwa nao kwenye mchezo wa Jumamosi kwa sababu ni wachezaji wenye uzoefu,” alisema Lwandamina.

Alisema kuwa pamoja na kuwakosa nyota hao, hiyo haiwezi kuwa sababu ya kupoteza mchezo huo na wamejipanga kupambana ili kupata pointi tatu.

“Naamini wachezaji ambao ninao wanaweza wakaifanya kazi nzuri Jumamosi..., tunaye Ajibu (Ibrahimu) na Chirwa (Obbrey) kwenye safu ya ushambuliaji ambao wamekuwa wakifanya vizuri,” alisema Lwandamina.

Aidha, Meneja wa timu hiyo, Hafidh Saleh, aliiambia gazeti la  Nipashe jana kuwa kikosi cha timu hiyo kinarejea Dar es Salaam leo mara baada ya mazoezi ya asubuhi tayari kuwakabili vinara hao wa ligi kuu.

“Hatuna majeruhi miongoni mwa wachezaji tulionao huku (Morogoro) na tunaomba wachezaji wandelee kuwa katika ari nzuri, tunarejea kesho (leo)asubuhi tutaingia kambini mpaka siku ya mchezo,” alisema Saleh.

Mchezo huo unatazamiwa kuwa na upinzani mkubwa hasa kutokana na ubora wa vikosi vya timu hiyo waliouonyesha kwenye michezo miwili iliyopita.
ads
Bonyeza HAPA kudownload applicationi ya SWAHILI NEWS kwenye simu yako ili kupata habari zetu Haraka
Share To:

SWAHIBA MEDIA STAFF

Habari , karibu katika mtandao wetu ili kuhabarika na stori zote za siku katika lugha yetu adhwim ya kiswahili, habarika wakati wote weka dunia kiganjani mwako na swahili news

Post A Comment: