MKUU wa Gereza la Segerea amewekwa njia panda juu ya matibabu ya mfanyabiashara Harbinder Sethi Singh, huku ikimtaka kumpeleka katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili ndani ya siku 14.


Amri hiyo ilitolewa jana na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, huku mkuu huyo wa gereza kutakiwa afike mahakamani kujieleza iwapo hatatekeleza agizo hilo.

Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi, alitoa amri hiyo baada ya wakili wa utetezi, Joseph Makandege, kuwasilisha maombi kwa mara ya nne kwamba mshtakiwa huyo bado anasumbuliwa na maradhi ya tumbo yanayosababishwa na puto alilowekewa.

Makandege alidai kuwa upande wa Jamhuri bado unaendelea kuidharau mahakama na kukiuka amri halali ya kuwataka kumpeleka mshtakiwa Muhimbili.

"Mheshimiwa Hakimu, upande wa Jamhuri unaitumia mahakama yako kuwakandamiza washtakiwa hasa wa kwanza (Sethi)  anateseka kwa sababu wamekiuka amri halali ya kumpatia matibabu stahiki.

Kama wameshindwa kumhudumia mshtakiwa hakuna sababu ya kuendelea kuwatesa mahabusu mahakama yako ifute mashtaka ili washtakiwa wapate haki yao ya msingi hasa matibabu," alidai Makandege.

Hata hivyo, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Leonard Swai, alidai kuwa upande wa Jamhuri unaomba mahakama iwape muda kwa ajili ya kushughulikia utaratibu wa kumpeleka mshtakiwa hospitali anayotaka.

" Mheshimiwa Hakimu, mahakama haitumiki kuwatesa washtakiwa, ilitoa amri kuhusu maombi ya utetezi lakini kuna utaratibu wa Jeshi la Magereza wa kutoa matibabu kwa mahahusu hata bila kuwa na amri yoyote," alidai Swai.

Swai alidai kuwa upande wa Jamhuri umejitahidi kuwasiliana na magereza namna ya kumpeleka Sethi Muhimbili na unaomba muda wa ziada wa kukamilisha utaratibu huo.

Hakimu Shaidi alisema mahakama yake ni sikivu imesikia maombi ya Jamhuri na kwamba mshtakiwa apelekwe Muhimbili ndani ya siku 14 .

"Mshtakiwa asipopelekwa Hospitali ya Muhimbili ndani ya siku 14, Mkuu wa Gereza la Segerea aje aileze mahakama kwa nini wameshindwa kumkamilishia huduma hiyo," alisema Hakimu Shaidi.

Alisema kesi hiyo itatajwa Oktoba 13, mwaka huu, na washtakiwa wataendelea kukaa mahabusu.

Mbali na Sethi, mshtakiwa mwingine ni James Lugemarila na wote wanakabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi na utakatishaji fedha.

Seth  na Rugemarila wanakabiliwa na mashtaka  12 ya  uhujumu uchumi  kwa kula njama, kujihusisha mtandao wa uhalifu , kughushi,  kutoa nyaraka za kughushi, kujipatia fedha kwa njia za udanganyifu,  kutakatisha fedha  na kuisababisha hasara ya dola za Marekani 22, 198,544.60 na Sh. 309,461,300,158.27.
ads
Bonyeza HAPA kudownload applicationi ya SWAHILI NEWS kwenye simu yako ili kupata habari zetu Haraka
Share To:

SWAHIBA MEDIA STAFF

Habari , karibu katika mtandao wetu ili kuhabarika na stori zote za siku katika lugha yetu adhwim ya kiswahili, habarika wakati wote weka dunia kiganjani mwako na swahili news

Post A Comment: