MBUNGE wa Jimbo la Arusha Mjini, Godbless Lema, amempongeza Rais John Magufuli, kwa kutoa mchango wa Sh. Milioni 260, kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za polisi 13 waliounguliwa moto Septemba 27.


Akizungumza jana na waandishi wa habari ofisini kwake, Lema ambaye ni Waziri Kivuli wa Mambo ya Ndani, alisema tukio la kuunguliwa polisi moto nyumba zao ni la kusikitisha na kumshauri Rais awajengee polisi wote Arusha na mikoa mingine nyumba bora.

“Hawa polisi ni walinzi wetu na wanafanya kazi kubwa ya kutulinda, lakini nyumba zao hazistahili kuishi binadamu ni kama zizi la ng’ombe, namshauri rais atenge bajeti ya kuwajengea polisi ghorofa au nyumba za hadhi yao,” alisema.

Alisema polisi kulingana na kazi zao wanazofanya hawastahili kufanyiwa harambee ya kujengewa nyumba, bali inatakiwa serikali kuamua kuboresha nyumba zao na miundombinu yao.

Aidha, alisema anatamani kutoa msaada, lakini kwa hali ilivyo sasa, anafahamu hautapokelewa.

Pia alimshauri Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba kujitafakari kama anafaa kuendelea kuwapo katika nafasi yake kutokana na matukio yanayoendelea nchini ya utekwaji watu na kupigwa risasi.

“Ben Saanane ametekwa na mpaka leo hajulikani alipo, sasa watawezaje kufanya uchunguzi wa tukio la kupigwa risasi Mwanasheria Mkuu wa Chadema Tundu Lissu na kuwapata wahusika, wakati hao wengine hawajafahamu, ndio maana tunataka wachunguzi wa nje ya nchi, lakini ajitafakari kama anafaa au la,” alisema.
ads
Bonyeza HAPA kudownload applicationi ya SWAHILI NEWS kwenye simu yako ili kupata habari zetu Haraka
Share To:

SWAHIBA MEDIA STAFF

Habari , karibu katika mtandao wetu ili kuhabarika na stori zote za siku katika lugha yetu adhwim ya kiswahili, habarika wakati wote weka dunia kiganjani mwako na swahili news

Post A Comment: