HATMA ya lini mshambuliaji Obbrey Chirwa ataanza kuitumikia Yanga, itajulikana leo baada ya kikao cha Kamati ya Maadili ya TFF ambacho kimemtaka nyota huyo kuhudhuria kikao hicho.


Uongozi wa Yanga umesema kuwa umepokea barua ya wito wa kuitwa Chirwa kwenye kikao cha Kamati ya Maadili ya TFF, ambayo itajadili suala lake la vurugu zilizotokea kwenye mchezo wa mwisho msimu uliopita dhidi ya Mbao FC katika Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.

Wakati hatma ya Chirwa ikisubiriwa, mshambuliaji Amissi Tambwe bado hali yake ya afya haijatengemaa na hivyo ataukosa mchezo wa Jumatano wa Ligi Kuu dhidi ya Njombe Mji.

Tambwe ambaye anasumbuliwa na maumivu ya mguu, hakucheza kwenye mchezo wa Ngao ya Jamii dhidi ya Simba na mchezo wa kwanza wa msimu mpya wa Ligi Kuu dhidi ya Lipuli ya Iringa, ambao walilazimisha sare ya bao 1-1 katika Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na gazeti la Nipashe jana, Meneja wa timu hiyo, Hafidh Saleh, alisema Tambwe bado hajaanza mazoezi, hivyo hatokuwapo kwenye kikosi kitakachosafiri Jumapili kwenda Njombe kwa ajili ya mchezo wao na Njombe Mji.

“Tambwe hawezi kusafiri na timu, bado hajapona, na kuhusu Chirwa hatma yake itajulikana kesho [leo] baada ya kikao na TFF, tumepokea barua leo (jana) ikimtaka Chirwa kufika TFF kesho (leo) saa nane mchana,” alisema Saleh.

Aidha, alisema timu hiyo mbali na kumkosa Tambwe, pia itawakosa Beno Kakolanya, Geofrey Mwashiuya ambao nao ni majeruhi.

“Kakolanya na Mwashiuya bado hawajapona na wanaendelea na matibabu nao pia hawatacheza mchezo ujao dhidi ya Njombe Mji,” aliongezea kusema Saleh.

Alisema wanategemea kuondoka Dar es Salaam Jumapili asubuhi kuelekea Njombe tayari kwa mchezo wao wa pili msimu huu.
ads
Bonyeza HAPA kudownload applicationi ya SWAHILI NEWS kwenye simu yako ili kupata habari zetu Haraka
Share To:

SWAHIBA MEDIA STAFF

Habari , karibu katika mtandao wetu ili kuhabarika na stori zote za siku katika lugha yetu adhwim ya kiswahili, habarika wakati wote weka dunia kiganjani mwako na swahili news

Post A Comment: