JE, unasumbuliwa na namna ya kupata njia rahisi ya kupunguza uwezekano wa kupata magonjwa yanayosumbua wengi kwa siku za hivi karibuni yakiwamo ya upungufu wa nguvu za kiume kwa kina baba, shinikizo la damu (presha) au chunusi mwilini?
Kama jibu ni ndiyo, basi habari njema ni kwamba ipo njia rahisi zaidi ya kukabiliana na maradhi hayo kabla hayajakufikia, nayo ni kutumia kwa mpangilio mzuri mchanganyiko wa asali na kiungo cha mdalasini.
Kwa mujibu wa ripoti mbalimbali za utafiti, na pia maelezo ya kitaalamu kutoka kwa Dk. Mshamu Abdallah Mwindah wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), ni kwamba mchanganyiko wa vyakula hivyo siyo tu husaidia kuwapunguzia walaji uwezekano wa kupata matatizo ya kiafya yanayohusiana na upungufu wa nguvu za kiume, presha na chunusi, bali pia husaidia kuukinga mwili wa mlaji dhidi ya magonjwa mengine zaidi ya 13.
Magonjwa mengine, ambayo ujio wake ndani ya mwili wa mwanadamu huweza kuzimwa kirahisi na mchanganyiko wa asali halisi na kiungo cha mdalasini ni uchovu wa mwili,
uzito mkubwa, uvimbe wa namna ya mabonge ya nyama mwilini, bakteria wanaosababisha harufu mbaya ya kinywa, tatizo la usikivu, kuvu (fungus), maumivu ya jino, mafua, maradhi ya moyo na pia tatizo la mchafuko wa tumbo utokanao na wingi wa gesi.
“Ni kweli. Mchanganyiko wa asali na mdalasini huwa na faida nyingi kwa mlaji, na hasa katika kumkinga dhidi ya magonjwa yatokanayo na kukithiri kwa mafuta mwilini,” alisema Dk. Mwindah wakati akizungumza na Nipashe mwishoni mwa wiki.
NAMNA VINAVYOSAIDIA
Akieleza juu ya siri ya asali na mdalasini katika kusaidia mwili kukabiliana na maradhi mbalimbali, Dk. Mwindah alisema chanzo chake ni aina ya virutubishio vilivyomo ndani ya vyakula hivyo.
Alisema asali imesheheni madini mengi yanayohitajika mwilini, yakiwamo ya magnesium na potassium. Kwa asili yake hiyo, asali husaidia kusisimua vichocheo vya mwili.
Kadhalika, alisema virutubishi vilivyomo katika mdalasini huwa na kazi nyingi mwilini ikiwamo ya kupunguza mafuta ghafi ambayo ndiyo huwa chanzo cha matatizo mengi yakiwamo ya uwezekano wa kupunguza nguvu za kiume kwa kina baba.
Kwa sababu hiyo, Dk. Mwindah alisema kuwa mchanganyiko wa vyakula hivyo, ndivyo mwishowe huleta faida kubwa katika mwili.
Akieleza zaidi, alisema mwili hutengeneza lehemu na vitu vya majimaji ambavyo vinaweza kugawanywa katika makundi makuu mawili, yaani vile ambavyo huhitajika kwa shughuli muhimu za mwili na vingine havihitajiki na kuwa adui wa mwili.
Virutubisho vingi vya asali na mdalasini, kwa mujibu wa Dk. Mwindah, husaidia kudhibiti vitu visivyohitajika mwilini ikiwamo kushusha kiwango cha lehemu.
“Mdalasini moja ya sifa yake ni kupunguza lehemu mwilini, inapunguza shinikizo la damu. Watu wenye kisukari huwa na tatizo kubwa la mishipa yao kujaa mafuta na hivyo kufanya mzunguko wa damu usifanyike vizuri,” alisema.
“Tatizo kubwa kwa watu wenye kisukari na presha huwa ni pamoja na kupungukiwa nguvu za kiume kutokana na mishipa yao ya damu kujaa mafuta.
“Na ili via vyao vya uzazi vifanye kazi vizuri, huhitajika kusimama baada ya mishipa ya damu kufikisha kiwango cha kutosha cha damu na kuufanya ubongo kusisimka. Mchanganyiko huu (asali na mdalasini) husaidia kufanikisha kazi hiyo,” alisema Dk. Mwindah.
Aidha, alisema vyakula hivyo husaidia pia wenye uzito mkubwa wa mwili na pia huondoa mabonge ya uvimbe wa nyama nje ya mwili.
“Wazee na wale wanaosumbuliwa na tatizo la uchovu wanashauriwa kunywa mchanganyiko wa mdalasini na asali kwa sababu ni tiba nzuri kwao,” alisema, kabla ya kutaja faida nyingine zikiwamo za kukinga mwili dhidi ya maradhi ya moyo kwa kuzuia kuwapo kwa mkusanyiko wa mtandao wa mafuta kwenye mshipa ya damu.
Alisema mchanganyiko huo ni tiba pia kwa watu wanaosumbuliwa na matatizo ya chunusi kwa sababu asali ina uwezo wa pekee wa kuua bakteria.
“Zipo faida nyingi kwa kwakweli. Na zote husaidia kuukinga mwili dhidi ya magonjwa mbalimbali,” alisema Dk. Mwindah, huku akitaja pia baadhi ya matatizo yanayozimwa na mchanganyiko huo kuwa ni pamoja na tatizo la kutoka harufu mbaya kinywani, tatizo la usikivu, kuvu (fangus), maumivu ya jino, mafua na kujaa gesi tumboni.
Post A Comment: